GWIJI WA WIKI: Mwalimu, mshairi na mwandishi chipukizi
Na CHRIS ADUNGO
UANDISHI ni mali na rasilmali iliyo kubwa, bora na yenye thamani zaidi kuliko rasilmali zote duniani. Kuwa na umilisi wa Kiswahili na kukitumia kwa ufasaha ni sawa na kujipa umiliki wa mgodi mkubwa wa dhahabu.
Kupitia uandishi, mtu anaweza kupata sifa na tija za kumfanya miongoni mwa binadamu wenye majina ya kipekee na ya kutajika katika ulimwengu wa utunzi. Anaweza pia kukutana na watu wengi zaidi ajabu katika sayari hii na pia kuzuru kwingi kutokana na kipawa chake hicho.
Kumiliki kipaji cha uandishi ni sawa na kuwa na ufunguo wa maisha – ufunguo usioweza kupotea wala kuibwa na mtu yeyote abadan kataan.
Milango ya heri imefunguliwa kwa weengi kupitia uandishi hasa katika Kiswahili na bado milango mingi inazidi kufunguka kwa chipukizi ambao siku zote wamepania kujihini na kujitolea sabili kufia na kuitetea lugha hiyo.
Kiswahili ni lugha hai yenye mawanda mapana yasiyoweza kabisa kuzuiliwa hata kwa chamchela, dhoruba, zilizala au kimbunga.
Huu ndio ushauri wa Bw Ayieko Sebastian Jakoyo – mwandishi chipukizi wa fasihi ya Kiswahili na mshairi shupavu ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Jiografia na somo la Biashara katika Shule ya Upili ya Kapkoimur, Kaunti ya Nandi.
MAISHA YA AWALI
Bw Jakoyo alizaliwa katika kijiji cha Nyapora, eneo la Mumias, Kaunti ya Kakamega akiwa mtoto wa kwanza kati ya sita katika familia ya Mama Leonora Nyaoro na Mzee Renson Jakoyo.
Alipata elimu ya shule ya msingi katika Shule ya Nyapora, Kata ya Koyonzo, Kaunti ya Kakamega kati ya mwaka 2000 na 2007. Alijiunga na Shule ya Upili ya St Peter’s Lubanga Mumias mnamo 2008 na kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mwishoni 2011.
Akiwa mwanafunzi wa shule ya upili, Jakoyo alichochewa kuandika na aliyekuwa mwalimu wake wa Kiswahili, marehemu Bw Wafula Kasili aliyemhimiza sana kuandika tungo mbalimbali za kubuni.
Kushiriki kwake kikamilifu katika Chama cha Kiswahili shuleni pia kulimsaidia pakubwa katika utunzi wa mashairi na hadithi fupi za kusisimua. Baadhi ya mashairi yamewahi kutia fora katika mashindano mbalimbali ya tamasha za kitaifa za muziki na drama miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi na upili.
ELIMU
Mnamo 2012, Jakoyo alijiunga na Chuo Kikuu cha Eldoret (Bewa Kuu) kusomea ualimu (Jiografia na somo la Biashara). Miongoni mwa wahadhiri waliofanikisha pakubwa safari yake ya katika taaluma ya ualimu ni Profesa Patrick Kafu, Dkt Titus Ochieng, Bw Richard Ochieng na Dkt Oseko.
Wahadhiri hawa walimpokeza malezi bora ya kiakademia hadi alipofuzu mwishoni mwa 2016.
Akiwa mwanafunzi wa chuo kikuu, Bw Jakoyo aliandika makala tofauti ya kibunifu na ya kitaaluma yaliyochapishwa katika majarida mbalimbali ya Kiswahili na Kiingereza.
Nyingi za kazi zake hata hivyo, zilikuwa hadithi fupi, mashairi na michezo ya kuigiza iliyochapishwa katika mitandao yake ya kijamii na gazeti rasmi la Chuo Kikuu cha Moi.
UALIMU
Baada ya kufuzu na kuhitimu Shahada ya Kwanza, Bw Jakoyo alianza kufundisha katika Shule ya Upili ya Konya, katika eneobunge la Ugenya, Kaunti ya Siaya kwa kandarasi aliyopokezwa na Halmashauri ya shule hiyo kuanzia mwezi Mei 2016 hadi Mei 2017.
Baadaye, alihamia Shule ya Upili ya Kapkoimur, Kaunti ya Nandi anakofundisha hadi sasa.
Kila mara anapowazungumzia wanafunzi wake darasani na hata baada ya vipindi vya masomo, Bw Jakoyo huwahimiza sana kuhusu umuhimu wa vipaji vya utunzi na upekee wa tija iliyomo katika kutambua, kulea na kukuza vipawa adhimu katika sanaa kwa ujumla.
Pia huwahamasisha zaidi wanafunzi kukitumia Kiswahili fasaha katika mazungumzo yao. Anawanasihi wanafunzi wake na wengi wengineo kujiepusha na matumizi ya lugha batini ambazo hulemaza makuzi na maendeleo ya Kiswahili na madhara yake ni matokeo mabaya katika somo hilo.
Kwa ushirikiano wake na walimu wa Kiswahili shuleni Kapkoimur – Bi Murindat Esleen, Bi Magut Juliet na Bw John Biwott (Mwalimu Mkuu), Bw Jakoyo amefaulu kukiasisi Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili Kapkoimur (CHAKIKA) ambacho hadi kufikia sasa kina jumla ya wanachama 200.
Walimu hawa wanamsaidia pakubwa kuwashauri wanachama wa CHAKIKA kwa nia ya kukuza vipawa vyao mbalimbali, kuwachochea kukithamini Kiswahili na kuwaelekeza vilivyo katika baadhi ya mada zinazowatatiza madarasani.
Chama hiki kinaenzi sana ubunifu miongoni mwa wanafunzi na huwa kinaanda mashindano ya mara kwa mara ya uandishi wa kibunifu miongoni mwa wanachama.
Mwalimu Mkuu pia amesaidia pakubwa katika kuwezesha uendeshaji wa shughuli za chama hiki kwa njia rahisi hasa ikizingatiwa wepesi wake katika kufadhili maandalizi na uhudhuriaji wa makongamano tofauti ya Kiswahili ndani na nje ya Shule ya Upili ya Kapkoimur.
UANDISHI
Bw Jakoyo alianza kuandika makala ya kibunifu akiwa mwanafunzi wa shule ya upili. Baadhi ya makala yake ni mashairi na hadithi fupi ambazo kwa wakati huo zililenga sana hadhira ya wanafunzi wenzake na walimu.
Baadhi ya mashairi yake yalichapishwa katika gazeti la shule. Alipojiunga na Chuo Kikuu cha Moi, alizidi kuandika makala za kitaaluma na kutunga mashairi yaliyolenga kujadili masuala yaliyohusu maisha halisi katika jamii iliyokuwa ikimzingira.
Baadhi ya kazi zake zilichapishwa katika toleo la kila muhula la ‘The Bridge’ ambalo ni gazeti rasmi la Chuo Kikuu cha Eldoret.
Bw Jakoyo alikuwa pia mwanachama wa Chama cha Kiswahili cha Chuo hicho na akaaminiwa wadhifa wa kuhariri makala ya kila Ijumaa yaliyokuwa yakichapishwa na Jarida la chama hicho.
Akiwa huko, bado aliandika michezo mbalimbali iliyoigizwa na kundi la Drama la chuo hicho liitwalo The Majirani Art Group. Baadhi ya michezo maarufu ya kuigiza aliyoiandika ni ‘Ua la Msimu’ na ‘Mfalme Mwoga’.
Mnamo 2017, mashairi ya Bw Jakoyo yalianza kuchapishwa katika kumbi za Ushairi Wenu na Sokomoko katika magazeti ya Taifa Leo na Taifa Jumapili.
Bw Jakoyo ana mkusanyiko wa mashairi ambayo kwa sasa yanashughulikiwa katika kiwango cha juu cha uhariri na hivi punde yatachapishwa katika kitabu.
Mbali na utunzi wa mashairi hasa kwa minajili ya mashairi ya tamasha za muziki kwa shule za msingi na upili,
Bw Jakoyo pia amekamilisha kuandika hadithi fupi ‘Ndoa ya Msimu’, ‘Usiku wa Giza’ na ‘Chozi la Mliwa’ ambazo zitafyatuliwa hivi karibuni na kampuni maarufu za uchapishaji wa vitabu humu nchini.
Akisisitiza kwamba uandishi wake unachochewa zaidi na Profesa Ken Walibora, Guru Ustadh Wallah Bin Wallah na Mohammed Khelef Ghassani, Bw Jakoyo ana ndoto ya kuchapisha makala na vitabu vingi zaidi vya Kiswahili vitakavyosomwa ndani na nje ya bara la Afrika.