• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Rais aagizwa na mahakama aapishe majaji walioteliwa

Rais aagizwa na mahakama aapishe majaji walioteliwa

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu umemwamuru Rais Uhuru Kenyatta kuwaapisha majaji 41 walioteuliwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kabla siku 14 zikamilike, kwani kutofanya hivyo ni ukiukaji wa katiba.

Katika uamuzi uliotolewa na Majaji Lydia Achode, James Makau na Enoch Chacha Mwita, Rais Kenyatta alikosolewa kwa kuchelewa kuapisha majaji hao waliohojiwa na kuidhinishwa na JSC.

Kesi hiyo iliwasilishwa na wakili mwanaharakati Adrian Kamotho ambaye alitaka korti imshurutishe Rais Kenyatta kuwaapisha majaji waliohitimu.

Katika uamuzi wao, walisema Rais hawezi kuhoji ama kubadilisha majina ya majaji aliyopelekewa kwa vile ni JSC iliyotunukiwa jukumu hilo la kuhoji, kuidhinisha ama kutoidhinisha yeyote ambaye ripoti zimesema yuko na dosari.

JSC iliwahoji na kuwateua majaji 41 mnamo Julai 2018 na kuwasilisha majina hayo kwa Rais Kenyatta atenge siku ya kuwaapisha lakini akadai “baadhi ya majaji walioteuliwa walikabiliwa na kashfa za ufisadi.”

Majaji walisema sio vyema kwa madai kutolewa kwamba miongoni mwa majaji walioteuliwa wanakabiliwa na madai ya ufisadi, bila kuwapa fursa ya kujieleza na kujiondolea lawama machoni mwa umma.

Mahakama ilisema kuwa sheria imetoa fursa kwa kila mmoja anayedaiwa kutekeleza jambo lililo kinyume cha sheria kujitetea.

“Ni ukandamizaji wa haki za mtu kudaiwa ni mfisadi na hapewi fursa ya kujitetea. Haki asili hutaka kila mmoja anayedaiwa alitenda jambo, apewe fursa ya kujiondolea lawama. Majaji waliodaiwa ni wafisadi hawakupewa nafasi ya kujitetea,” walisema Majaji.

Majaji hao walisema kutoapishwa kwa majaji hao kunasababisha mrundiko wa kesi katika mahakama ya rufaa, mahakama kuu, mahakama ya kuamua mizozo ya wafanyakazi (ELRC) na mahakama ya kuamua kesi za ardhi (ELC).

Kupitia kwa wakili Paul Muite, JSC iliwaomba majaji hao watatu wamwamuru Rais Kenyatta atekeleze majukumu yake ya kikatiba.

Mnamo Julai 22, Jaji Mkuu David Maraga alimpelekea majina ya Majaji 11 waliohitimu kuhudumu katika mahakama ya rufaa, majaji 20 katika mahakama kuamua kesi za mashamba na majaji 10 kuhudumu katika korti ya kuamua mizozo ya wafanyakazi na waajiri.

You can share this post!

Serikali yatoa ratiba ya safari ya kumuaga Moi

Vyama vidogo vyadai kupuuzwa katika BBI

adminleo