Kimataifa

Jumla ya watu 563 wamekufa kutokana na virusi vya Corona

February 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA AFP

IDADI ya watu ambao wamefariki kutokana na maradhi ya Homa ya China Alhamisi ilipanda kwa siku tatu mfululizo hadi kufikia watu 563 nchini China huku wataalamu wakiimarisha juhudi za kusaka tiba ya ugonjwa huo hatari.

Mkurupuko wa virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa huo umekwamisha shughuli katika miji kadhaa nchini China huku watu kadhaa wanaokisiwa kuambukizwa virusi hivyo kulazwa katika wadi zilizotengwa.

Katika mkoa wa Hubei, vifo 70 vipya viliripotiwa Jumatano jioni huku maambukizi 2, 987 mapya yakithibitishwa.

Vifo vingine viliripotiwa katika mji wa Tianjin ulioko mkoa wa Heilongjiang na katika mkoa wa Guizhou ulioko kusini mashariki mwa China.

Katika mji wa Wahan ambako virusi vya kwanza viliripotiwa, shughuli zimekwama kwa zaidi ya wiki mbili huku vituo vya treni, viwanja vya ndege na barabara zikifungwa.

Kuna vifo viwili vilivyoripotiwa nje ya China, nchini Ufilipino na jimbo la Hong Kong, vya watu walioaminika kutoka jijini Wuhan.

Mamia ya wageni wamehamisha kutoka jiji hilo na kuwekwa katika kituo maalum kote ulimwenguni. Na abiria na wahudumu katika meli nchini Japan na Hong Kong walizuiwa katika vyombo hivyo.

Watu kumi zaidi katika meli kwa jina Diamond Princess katika bandari ya Yokohama, kusini mwa Tokyo waligunduliwa kuwa na virusi vya corona, wizara ya afya ilisema.

Jumla ya watu 3,700 wamezuiliwa katika chombo hicho baada ya mzee mwenye umri wa miaka 80 raia wa Hong Kong aliyeiabiri mwezi jana kupatikana na virusi hivyo.