Wachina watiwa adabu kwa kushambulia Mkenya
Na RICHARD MUNGUTI
RAIA wanne wa Uchina miongoni mwao mpishi aliyenaswa katika picha za video akimshambulia raia wa Kenya na kumwumiza watakaa rumande siku tatu polisi wakamilishe uchunguzi.
Hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Nairobi, Bi Hellen Onkwani, aliamuru Deng Hailan, Ou Qiang, Yu Ling na Chang Yueping wazuiliwe katika kituo cha Polisi cha Kilimani kuhojiwa na kuandikisha taarifa walichokuwa wanafanya nchini bila ya kuwa na hati za kuwaruhusu kufanya kazi nchini.
Wanne hao waliokuwa wanashika mapua wakiwa ndani ya korti na pia wakipelekwa kuabiri gari la polisi watakula maharagwe hadi Februari 13, 2019 watakaporudishwa kortini ujumbe utolewe ikiwa uchunguzi umeumbua walichokuwa wanafanya nchini.
Bi Onkwani alifahamishwa Polisi waliwatia nguvuni kufuatia malalamishi ya umma walioeleza ghadhabu yao kufuatia dhuluma waliyoshuhudia ikitendewa Bw Simon Osako Silo.
Bw Silo aliyepata kichapo cha mbwa aliwasilisha ripoti katika kituo cha polisi cha Kileleshwa jinsi alishambuliwa na Deng Hailan, kwa kufika kazini akiwa amechelewa mnamo Feburuaru 2, 2020.
Baada ya kupata kichapo cha nguruwe, Bw Silo alitumuliwa kazini na Polisi wanaendelea kumsaka aandikishe taarifa kufuatia kutiwa nguvuni kwa wanne hao.
Wakiwasilisha ombi la kutaka washukiwa hao wazuiliwe kwa siku 21 , vongozi wa mashtaka Jacinta Nyamosi na Everlyn Onuga walieleza korti , “ inahofiwa washukiwa watatoroka endapo wataachiliwa kwa dhamana.”
Mahakama ilielezwa Polisi watawasiliana na Idara nyingine za Serikali kama vile Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA) kubaini ikiwa wanne hao walikuwa wanalipa kodi kutokana na ajira yao.”
Mahakama ilielezwa uchunguzi uliofanywa kufikia sasa umebaini Deng, Qiang na Yueping ni wapishi ilhali Ling ni mhasibu katika Mkahawa huo.
Hati za idara ya uhamiaji walizokuwa nazo wanne zilionyesha “walikuwa wameingia nchini kama Watalii na hawana hati kutoka idara ya Uhamiaji wa kukubaliwa kufanyakazi ya Upishi nchini.”
Bi Onkwani alielezwa, Deng Hailan ambaye ni mshukiwa mkuu katika kesi watakayofunguliwa ni Mpishi katika hoteli ya Chez Wou Restaurant iliyoko mtaa wa Kileleshwa, Kaunti ya Nairobi.
Hoteli hiyo uandaa vyakula vya Kichina na Bw Silo alikuwa ameajiriwa katika hoteli hiyo.
Hakimu aliombwa aamuru washukiwa hao wazuiliwe kwa siku 21 ndipo kaunti ya Nairobi ibaini ikiwa ilikuwa imeipa hoteli hiyo kibali cha kuendeleza biashara ya vyakula jijini.
Mahakama iliombwa iwazuilie washukiwa hao ndipo idara kadhaa za Serikali zitoe ripoti zao kuwahusu washukiwa hao wanne kabla ya mashtaka dhidi yao kutayarishwa.
Miongoni mwa mashtaka ni kumpiga na kumjeruhi, kuendeleza biashara ya hoteli bila leseni, kutotekeleza masharti ya Visa walizopewa mwaka jana walipoingia nchini na muda wake umeyoyoma na kuwako nchini bila kibali.
Washukiwa hao waliamriwa warudishwe kortini siku moja kabla ya sikukuu ya Valentine.