Baadhi ya madereva wadai hafla ya kitaifa imewaondolea usumbufu wa maafisa
Na MAGDALENE WANJA
WAHUDUMU wa biashara ya matatu jijini Nairobi wamepata afueni Jumanne kwa kile wamesema ni kuwepo kwa maafisa wachache wa trafiki barabarani.
Kulingana na baadhi ya wahudumu, hafla ya maombi maalum ya kitaifa kumuenzi Rais mstaafu Daniel Arap Moi aliyefariki Jumanne wiki jana imewapa afueni kwani maafisa wengi ambao huwanyanyasa barabarani walikuwa wamepewa kazi ya doria na majukumu mengine katika sehemu za hafla.
“Wengi wa maafisa wa trafiki hupenda kuchukua hongo bila makosa yoyote na tulipopata kuwa wengi hawapo leo Jumanne, tumefurahi sana,” amesema Bw *Tony ambaye anahudumu katika barabara ya Thika Superhighway.
Wahudumu hao wamesema kuwa maafisa hao huwa wakali mwingi siku ya Jumatatu baada ya wikendi ambapo huitisha hongo hata kuanzia Sh400.
“Maafisa hawa huwa tishio kubwa hasa unapokosa kulipa kiwango wanachoitisha na unaweza ukakamatwa kwa makosa ya kusingiziwa.
Wameongeza kuwa kuondolewa kwa baadhi ya mafisa hao barabarani kumewafaa zaidi.
Kilele cha kumuaga Moi kinatarajiwa Jumatano atakapozikwa Kabarak katika Kaunti ya Nakuru.
Watumiaji wa barabara ya Mumias-Busia mnamo Jumatatu walilalamika wakisema wanahangaishwa sana na maafisa wa trafiki eneo la Ejinja wakidai wanaitisha hongo.