• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Ni mavazi ya KANU pekee yataruhusiwa kwa mazishi ya Moi – Serikali

Ni mavazi ya KANU pekee yataruhusiwa kwa mazishi ya Moi – Serikali

Na CHARLES WASONGA

WAKENYA wameonywa dhidi ya kuvalia mavazi yenye rangi za vyama vya kisiasa watakapohudhuria hafla ya mazishi ya marehemu rais wa zamani Daniel Arap Moi nyumbani kwake Kabarak Jumatano.

Kwa mujibu wa Mshirikishi wa Rift Valley George Natembeya, ikiwa yeyote anahisi kwamba sharti avalie mavazi ya chama cha cha kisiasa, basi shati lake liwe na nembo ya KANU; chama ambacho marehemu alijihusisha nacho hadi alipostaafu siasa mnamo 2002.

“Hii sio shughuli ya kisiasa, usije hapo ikiwa umevalia tishati ya BBI au chama chochote cha kisiasa. Ikiwa shari uvalie mavazi ya vyama vya kisasa, basi valia yale ya Kanu pekee,” akasema Jumanne kwenye kikao na wanahabari mjini Nakuru.

Bw Natembeya alisema matayarisho ya hafla hiyo yamekamilishwa na jumla ya watu 30,000 wanatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo ya kitaifa.

Hata hivyo, alifafanua kwamba ni watu 500 pekee, hususan watu wa familia, wataruhusiwa kufika karibu na kaburi.

Bw Natembeya aliwataka wananchi wanaotaka kuhudhuria mazishi hayo kuwa wamewasili mwendo wa saa moja asubuhi kwani ratiba kamili itaanza saa tatu asubuhi.

Mnamo Jumatatu, Bw Natembeya alisema waombolezaji watapewa soda, mkate na nakala ya ratiba watakapowasili nyumbani kwa Mzee Moi.

Hata hivyo, baadhi ya Wakenya mitandaoni walisisiza kuwa sharti wapewe “lishe kamili” katika mazishi ya Rais mstaafu wakisisitiza kuwa Mzee Moi alikuwa kiongozi mkarimu.

Bw Natembeya alisema hema kubwa zimetundikwa katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Kabarak ambako ibada ya mazishi itaendeshwa.

“Zaidi ya viti 30,000 vimewekwa katika mahema na vitatumiwa na wananchi watakaohudhuria mazishi ya Mzee Moi. Na kuna nafasi ya kutosha watu zaidi,” akasema.

Afisa huyo aliongeza kuwa mabasi yote ya shule katika kaunti ya Nakuru yamekodiwa kuwasafirishwa watu hadi Kabarak.

“Serikali ya kaunti ya Nakuru pia itachangia magari mengine,” Bw Natembeya akasema, huku akiongeza kuwa magari hayo yataanza kuwasafirisha watu kuanzia saa kumi na nusu alfajiri Jumatano.

You can share this post!

NGILA: Usalama mitandaoni unahitaji ushirikiano kimataifa

Wabunge walivyoimba nyimbo za kusifu Nyayo bungeni

adminleo