• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Museveni alivyowavunja mbavu Wakenya

Museveni alivyowavunja mbavu Wakenya

Na PETER MBURU

RAIS wa Uganda Yoweri Museveni jana aliwachangamsha Wakenya pamoja na wageni waliohudhuria ibada ya wafu ya kumuaga Rais Mstaafu Daniel arap Moi, kwa rambirambi zake ambazo ziliibua ucheshi mara kwa mara.

Katika hotuba yake ya takriban dadika nane, Rais Museveni alimmiminia Mzee Moi sifa, akimtaja kuwa kiongozi aliyedumisha amani Kenya, aliyependa kutatua mizozo na aliyepigania umoja wa Afrika Mashariki.

Rais Museveni alisema kuwa ni sifa hizo ambazo zinamfanya Mzee Moi kusherehekewa hadi sasa, kwani kinyume na Uganda iliyokumbwa na vita kwa miaka kadhaa, Kenya imekuwa na amani tangu ilipopata uhuru.

“Kifo kwa binadamu ni lazima; tofauti ni kujibu swali ‘umefariki baada ya kufanya nini?’. Kama ulifanya mambo ovyo…baas, tunakusahau au tunakukukumbuka kwa mabaya uliyofanya.

“Kenya mmekuwa kwa amani tangu mlipopata uhuru, hamjapata vita na misukosuko isipokuwa michache tu iliyotokea hapa iliyokuwa kama mchezo tu,” akasema Rais Museveni, matamshi yaliyowachekesha waliohudhuria.

Rais huyo aliendelea kutoa historia ya jinsi Mzee Moi alivyokuwa miongoni mwa waliovunja chama cha Kadu ili kujiunga na Kanu mnamo 1964, akisema hatua hiyo ilihakikisha kuwa Kenya ilisalia kwa umoja.

“Mnakumbuka… nyinyi? hamkumbuki! nyinyi ni watoto wadogo. Sisi ambao tulikuwapo tunajua palikuwapo vyama vya Kanu na Kadu. Mnamo 1964, Mzee Moi na wenzake waliokuwa Kadu walijiunga na Kanu na kukifanya chama kimoja. Hiyo inamaanisha walikuwa wamegundua umuhimu wa umoja na hiyo ilisaidia Kenya kusalia na amani miaka hii yote,” akasema, akiendelea kuwachekesha watu.

Rais Museveni pia alikumbuka jinsi Mzee Moi alivyowahi kufunga mpaka wa Kenya na Uganda baada ya kuchochewa wakati yeye (Museveni) alipoingia uongozini, lakini baadaye akakubali kuufungua.

“Baada ya sisi kuingia kwa serikali kule, wafanya-fujo wakawa wanamdanganya hapa kuwa sisi si watu wazuri… Mzee Moi akakasirika nasi na akafunga mpaka lakini baadaye tukapatana na Wateso wa Kenya na tukamaliza hiyo shida yote,” akasema.

Akiashiria kuwa Mzee Moi alikuwa kiongozi mwema kwa Kenya, alisema barani Afrika viongozi ni dawa na kuwa wanatibu matatizo ya nchi zao, akisema Kenya ilipata viongozi wema.

“Waganga wenu hapa, viongozi wenu waligundua ugonjwa wenu na wakawapa dawa inayofaa. Mzee Moi pamoja na Mzee wetu wa zamani Kenyatta walikuwa na dawa iliyotibu shida za Kenya na za Afrika Mashariki. Dawa ya kwanza ilikuwa uzalendo ndani ya Kenya,” akasema.

Vilevile, alikumbuka jinsi wakati mmoja Mzee Moi alivyomuomba kumpeleka katika kanisa moja la AIC nchini Uganda, katika eneo la Arua.

You can share this post!

Moi alizingatia uaminifu kuliko kiwango cha elimu

Viongozi wa mataifa 7 wahudhuria ibada ya mwisho ya Moi

adminleo