• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Viongozi wa mataifa 7 wahudhuria ibada ya mwisho ya Moi

Viongozi wa mataifa 7 wahudhuria ibada ya mwisho ya Moi

Na LEONARD ONYANGO

VIONGOZI 7 wa mataifa mbalimbali ya Afrika walikuwa miongoni mwa maelfu ya Wakenya waliofika katika uwanja wa Nyayo kwa ajili ya ibada ya kumuaga Rais Daniel arap Moi.

Miongoni mwa viongozi wa Afrika waliohudhuria ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Paul Kagame (Rwanda), Rais Ismail Omar Guelleh (Djibouti), Rais Salva Kiir (Sudan Kusini), Rais Sahle-Work Zewde (Ethiopia), Rais Brahim Ghali (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Sahrawi) na marais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

Wengine ni Naibu Rais wa Nigeria Yemi Osinbajo, Naibu Rais wa Namibia Nickey Iyambo, waziri wa Masuala ya Kigeni wa Burundi Alain Aime Nyamitwe kati ya wengineo.

Kulingana na Wizara ya Masuala ya Ndani wakuu wa mataifa 10 wanatarajiwa kuhudhuria leo hafla ya mazishi ya Mzee Moi katika eneo la Kabarak, Kaunti ya Nakuru.

Akihutubu uwanjani Nyayo, Rais Kagame alimtaja Mzee Moi kama kiongozi shupavu aliyepigania umoja wa Afrika Mashariki.

Wakati wa utawala wa Moi, uhusiano baina ya Kenya na Rwanda ulidorora kwa muda kufuatia madai kwamba Kenya ilificha baadhi ya Wahutu waliotekeleza mauaji ya halaiki dhidi ya Watutsi mnamo 1994.

Uhusiano huo ulififia zaidi Waziri wa Masuala ya Ndani wa Rwanda, Seth Sendashonga na dereva wake, walipouawa mnamo Mei 1998 katika barabara ya Limuru-Forest (ambayo sasa inajulikana kama Wangari Maathai) mtaani Parklands jijini Nairobi.

Rais Kagame alizanzisha juhudi za kufufua uhusiano huo alipoingia mamlakani mnamo 2000.Rais Museveni alimtaka Moi kama mzalendo aliyedumisha amani nchini Kenya.“Rais Moi alikuwa mzalendo aliyeunganisha Wakenya.

Alipenda kuona mataifa ya Afrika Mashariki yameungana. Hata wakati mmoja alipendekeza tubuni Shirikisho la Afrika Mashariki,” akasema Rais Museveni.

“Kuna wakati kulikuwa na tofauti baina ya Kenya na Uganda kiasi kwamba Rais Moi alifunga mpaka. Lakini baadaye tulikutana tukamaliza tofauti kwa hiyo Mzee Moi alikuwa mpatanishi,” akaongezea.

Kiongozi wa Uganda pia alielezea jinsi Rais Moi alimtaka ampeleke katika Kanisa la Africa Inland (AIC) lililoko katika eneo la Arua, Kaskazini mwa Uganda.

Katika risala zake za rambirambi alizotoa Jumanne wiki iliyopita, Rais Museveni alisema: “Nilikutana na Mzee Moi kwa mara ya kwanza miaka ya 1970 nilipokuwa mwanafunzi katika Chuo kikuu cha Dar es Salam akiwa Makamu wa Rais.”

Wawili hao walikutana kwa mara ya pili katika kongamano mjini Arusha, Tanzania mnamo 1985 Mzee Moi akiwa rais huku Museveni akiwa waziri.

Rais Mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete alisema: “Nilimfahamu Rais Moi tangu nilipokuwa shuleni. Nilipoteuliwa kuwa waziri wa Kawi na Madini, Rais Ali Hassan Mwinyi alinituma kwa Mzee Moi kufanya mazungumzo naye kuhusu pendekezo la kujenga bomba la gesi kutoka Dar es Salaam hadi Kenya,.

“Nilipofika nchini Kenya Rais Moi alinipokea kwa furaha. Alifurahia pendekezo hilo na baada ya mazungumzo alinisindikiza kutoka afisini kwake hadi ndani ya gari. Amenifunza kuhusu namna ya kuheshimu watu,” akaongezea.

Mtangulizi wake Benjamin Mkapa aliyeongoza ujumbe kutoka Tanzania alisema: “Rais John Magufuli ametutuma sisi wawili kuthibitisha ukaribu wa dhati kati ya Tanzania na Kenya.Nilikuwa rais kwa miaka kumi na saba nilifanya kazi na Rais Moi.”

Rais Moi alifufua Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baada ya kuporomoka mtangulizi wake Jomo Kenyatta walipotofautiana na mwenzake wa Tanzania Julius Nyerere.

Moi alizuru Tanzania kwa mara ya kwanza akiwa rais mnamo Novemba 16, 1983 kwa njia ya barabara..Siku hiyo aliafikiana Nyerere kufungua tena mpaka na huo ndio ulikuwa mwisho wa uhasama baina ya Tanzania na Kenya.

Mnamo Julai 9, 2011, Sudan Kusini ilipopata uhuru wake kutoka kwa Sudan, maelfu ya raia wa nchi hiyo walishangilia jina la Mzee Moi lilipotajwa.Rais Moi alihudhuria hafla hiyo ya kusherekea uhuru iliyofanyika katika uwanja wa Dr John Garang Mausoleum.

Mzee Moi alikuwa miongoni mwa viongozi walioshiriki katika mazungumzo ya kutenganisha mataifa hayo mawili.Jana, Rais Kiiri alisema: “Nchi ya Sudan Kusini ni matunda ya juhudi za Mzee Moi.”

You can share this post!

Museveni alivyowavunja mbavu Wakenya

Rais ataja marehemu Moi kama shujaa

adminleo