Habari Mseto

Wakuu wa vyuo vya kiufundi waonywa dhidi ya kuongeza karo kila mara bila kuifahamisha TTI

February 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na BRENDA AWUOR

WAKUU wa vyuo vya kiufundi katika kaunti za Kisumu, Siaya, Migori, Busia, Homa Bay, Kisii, Nyamira, Bungoma, na Kakamega wameonywa vikali dhidi ya kuongeza karo kila mara bila kujulisha taasisi inayosimamia vyuo vya kiufundi.

Katika mkutano ulioandaliwa baina ya wakuu wa vyuo vya kiufundi na shirika la USAID eneo la chuo cha kiufundi Kisumu, wasimamizi hao wakiongozwa na Afisa mkuu Bw Kevit Desai, walionya wakuu hao dhidi ya kuongeza karo kila mara ikiwa ni kinyume cha sheria na kanuni za TTI.

Bw Desai alieleza kuwa karo halisi ambayo kila mwanafunzi anastahili kulipa ni elfu Sh56,000 kwa mwaka huku serikali ikilipia kila mwanafunzi Sh 30,000 na mwanafunzi binafsi kulipa Sh26,000.

Bw Kevit Desai akihutubia wanahabari. Picha/ Elizabeth Ojina

”Karo halisi katika vyuo vya kiufundi vyote ni Sh56,000 kwa mwaka na ambapo serikali hulipia kila mwanafunzi takribani Sh30,000 na mwanafunzi akitarajiwa kulipa Sh26,000 zinazosalia,” alieleza.

Wazazi wamehimizwa kuchukua hatua na kuhakikisha kuwa kila mtoto baada ya kidato cha nne amejiunga na chuo kikuu au chuo cha kiufundi chochote.

Alishauri wale ambao wana tatizo la karo kutembelea ofisi za Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (Helb) ili wapewe mkopo wa kutosha kujielimisha.

”Watoto mayatima pamoja na wale ambao hawawezi kugharimia karo ya vyuo, watafute mkopo kutoka Helb ambayo itawapa Sh40,000 kwa mwaka na kugharimia karo pamoja na mahitaji mengine,” alihitimisha.

Onyo hili limekuja wiki mbili baada ya wanafunzi kutoka chuo cha kiufundi cha Kisumu kuandamana na kusababisha kufungwa kwa chuo.

Waliogoma walilalamikia kuongezeka kwa karo na ukosefu wa usalama wa kutosha.