• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 10:55 AM
Mwili wa mvuvi aliyetoweka wapatikana Ziwa Victoria

Mwili wa mvuvi aliyetoweka wapatikana Ziwa Victoria

Na BRENDA AWUOR

MWILI wa mvuvi wa kiume aliyetoweka Alhamisi jioni umepatikana Ziwa Victoria Ijumaa asubuhi hiii ikiwa ni baada ya juhudi za pamoja zilizofanywa na wavuvi wengine kutoka Kisumu.

Willis Onyango aliyekuwa na umri wa miaka 38, alipotea Alhamisi jioni baada ya kutoka nyumbani kwake na kuelekea ufuo wa Ngege, Kisumu ili kuongelea majini kama alivyozoea.

Mkazi wa kaunti ndogo ya Korando, Kisumu, akiwa na mazoea na kuogelea maeneo hayo kila siku, alikumbana na kifo chake baada ya boti yake kupinduliwa na upepo mkali ziwani.

Walioshuhudia kitendo hicho walieleza kuwa boti ya Bw Onyango ilizama majini kutokana na upepo mkali wakati huo.

Walijaribu kuitisha msaada ila hakukuwa na yeyote wa kuingia majini ili kuokoa maisha ya marehemu.

Chifu wa eneo hilo Bw Simon Osego, kwa kuongea na ‘Taifa Leo’ kwa simu, amesema kuwa alitambua mwili huyo kuwa ni wa Bw Onyango aliyetoweka Alhamisi jioni.

”Marehemu alitoka kwake kuelekea maeneo ya Ngege ambapo yeye huogelea kila siku baada ya kumaliza kazi ya uvuvi,” ameeleza chifu.

Nduguye marehemu, Bw Steve Otieno, ameeleza kuwa Bw Onyango alikuwa na mazoea ya kupeleka samaki sokoni kila siku baada ya kumaliza uvuvi kisha kurudi tena huko kuogelea.

”Baada ya kumaliza kuvua samaki, angesafirisha samaki sokoni kisha kurudi maeneo hayo kuoga,” nduguye ameeleza.

You can share this post!

Mkandarasi wa ujenzi barabara ya Lamu-Garsen asitisha...

MWANAMKE MWELEDI: Jina lake halikosi sekta ya biashara

adminleo