HabariSiasa

Echesa asukuma Ruto kona mbaya

February 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na LEONARD ONYANGO

NJAMA ya utapeli kuhusu ununuzi wa silaha iliyopelekea aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa kukamatwa wiki iliyopita, imemfanya Naibu Rais William Ruto kubanwa zaidi.

Sakata hiyo imewapa wapinzani wake katika siasa fursa ya kumshambulia wakimtaka ajiuzulu.

Jumapili, wabunge wa ODM John Mbadi na Opiyo Wandayi walisema Naibu Rais anapasa kujiondoa madarakani, mwito ambao pia uliungwa mkono na Gavana Charity Ngilu wa Kitui.

Kwenye taarifa, Bi Ngilu alisema msimamo wa Dkt Ruto kupitia Twitter ni dhihirisho kwamba alifahamu yale yaliyokuwa yakiendelezwa na washukiwa afisini mwake.

“Hali hii imeaibisha nchi na afisi ya Rais. Hii si mara ya kwanza ambapo afisi ya Ruto inatajwa katika kashfa ya aina hii,” akasema Bi Ngilu.

Lakini Kinara wa Wengi katika Bunge la Taifa Adan Duale na mwenzake wa Seneti Kipchumba Murkomen walimtetea Dkt Ruto na kutaka Kiongozi wa ODM Raila Odinga pia achunguzwe kuhusu sakata ya dhahabu feki ya mwaka jana.

Dkt Ruto alishutumu Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) na akataka kupewa majibu kuhusu sakata hiyo inayohusu kandarasi ya vifaa vya kijeshi vya thamani ya takriban Sh40 bilioni.

Dkt Ruto alijitokeza kujitetea baada ya kubainika kuwa watu wawili ambao ni raia wa kigeni, walienda afisini kwake wakiandamana na Bw Echesa kujadili kandarasi ya silaha za kijeshi.

Jumapili, Dkt Ruto alionekana kuashiria kwamba sakata hiyo ilihusisha afisi nyinginezo kuu serikalini.

Aliwataka wapelelezi kueleza Wakenya afisi zote ambazo walaghai hao walizuru kabla ya kwenda afisini kwake wiki iliyopita kwani, kulingana naye, kutofanya hivyo itakuwa ni kuingiza siasa katika suala hilo ili ionekane anahusika katika utapeli huo.

“Afisi ya Naibu wa Rais haiagizi bidhaa au vifaa kwa ajili ya wizara za serikali,” akasema Dkt Ruto.

“Mipango ya utapeli huo ilifanyika kwa miezi mingi, lakini walienda afisini kwangu kwa dakika 23 pekee. Je, matapeli hao walizuru afisi zipi zingine kabla ya kwenda ofisi yangu Harambee Annex,” akongezea.

Dkt Ruto pia anataka kujua ikiwa wawekezaji hao walizuru Makao Makuu ya Jeshi (DoD) au la: “Na walikutana na nani huko DoD? Tafuteni ukweli,” akasema Dkt Ruto.

Ununuzi wa vifaa vya kijeshi hufanywa kwa usiri mkubwa na ustadi wa hali ya juu ukihusisha idara kadhaa katika serikali kuu.

Bw Echesa, ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto kisiasa, alikamatwa Alhamisi iliyopita na anatarajiwa kuachiliwa huru leo jioni kwa dhamana ya Sh1 milioni baada ya maafisa wa uchunguzi kukamilisha shughuli ya upekuzi nyumbani kwake.

Mnamo Ijumaa, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) Lucas Onyina, aliagiza Bw Echesa awekwe rumande katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga, Nairobi, hadi leo kuruhusu maafisa wa uchunguzi kufanya upekuzi nyumbani kwake kwa lengo la kutafuta ushahidi zaidi kuhusiana na sakata hiyo.

Upekuzi huo pia utafanyika katika nyumba za washtakiwa wenzake Daniel Otieno, Clifford Okoth na Kennedy Oyoo Mboya.

Wawekezaji wa kampuni ya Eco Advanced Technologies walidai kuwa Bw Echesa aliwaahidi kuwa angetumia ushawishi wake serikalini kuwasaidia kupata kandarasi ya kuuzia Kenya vifaa vya kijeshi.

Inadaiwa kuwa wawekezaji hao kutoka Poland walikuwa wamelipa Sh50 milioni za kufanikisha kupata kandarasi hiyo.

Alhamisi wiki iliyopita, washukiwa hao walifika katika afisi ya Naibu wa Rais katika majengo ya Harambee House Annex wakitaka kukutana na Dkt Ruto.

Baada ya kufahamishwa kuwa Dkt Ruto hakuwepo, waliondoka lakini wakakamatwa na maafisa wa DCI.

Afisi ya Naibu wa Rais imekiri kwamba wawekezaji hao wakiwa wameandamana na Bw Echesa walifika afisini hapo mnamo Februari 13, mwaka huu, lakini Dkt Ruto hakuwepo.

Kulingana na DCI, Bw Echesa alienda Poland akiandamana na mtu aliyejiita kamanda wa Jeshi kwa jina Mohammed Sabu kukagua vifaa vya kijeshi nchini Poland.

Sabu, ambaye katika afisi ya Dkt Ruto anajulikana kama ‘Otieno’ pamoja na Echesa, wamekuwa wakifanya vikao na wawekezaji hao Nairobi.

Habari za ziada na Justus Ochieng na Kitavi Mutua