Habari MsetoSiasa

Chebukati alaumu BBI kwa kupuuza maoni ya IEBC

February 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati amelaumu jopo la Mpango wa Maridhiano (BBI) kwa kupuuza mapendekezo ya tume hiyo.

Bw Chebukati amesema licha ya kuwa IEBC ilialikwa mara mbili mwaka uliopita kuwasilisha mapendekezo kuhusu marekebisho yanayohitajika kwa usimamizi wa uchaguzi nchini, maoni waliyotoa hayamo kwenye ripoti ya BBI.

Ripoti hiyo ilizinduliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Novemba mwaka uliopita katika ukumbi wa Bomas, Nairobi, katika hafla iliyohudhuriwa pia na naibu wake William Ruto na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

“Tume ilipokea mwaliko kutoka kwa jopo la BBI, ikawasilisha maoni yake mara mbili. Mara ya kwanza ilikuwa katika kikao cha wazi kisha mara ya pili ikawa faraghani. Lakini mapendekezo ya tume hii yalipuuzwa kabisa na jopo hilo kwani hayakujumuishwa katika ripoti,” akasema.

Alisema hayo kwenye nakala mpya iliyowasilishwa na IEBC kwa jopo la BBI ambalo liliongezwa muda na Rais Kenyatta ili kupokea mapendekezo kutoka kwa umma kuhusu ripoti yao.

“Kutokana na kuwa jopo la BBI liliongezwa muda, tume hii imepata nafasi ya kuwasilisha mapendekezo yake upya,” akasema Bw Chebukati.

Licha ya kuwa alipinga mapendekezo mengi yaliyomo kwenye ripoti hiyo kuhusu usimamizi wa uchaguzi, Bw Chebukati alikubali kwamba inahitajika maafisa wakuu wote wa tume wapigwe msasa upya.

Alisema ingawa tume hufuata sera kali na sheria za uadilifu inapoajiri wafanyakazi wake, wamejitolea kufanyiwa uhakiki ili kuondoa dhana kwamba wao hukiuka sheria wanaposimamia uchaguzi.

“Kutokana na madai yanayoenezwa mara kwa mara na baadhi ya wanasiasa kwamba tunahusika katika ukiukaji wa sheria za uchaguzi, tume hii haina pingamizi kuhakiki maafisa wake wakuu,” akasema.

Hata hivyo, aliongeza kuwa ni sharti kama shughuli hiyo itafanywa iwe kwa njia wazi na ya haki.

Tume hiyo imepinga mapendekezo kadhaa ya BBI kama vile kuruhusu wanasiasa kuchagua makamishna wa IEBC.

Mwenyekiti huyo alisema pendekezo hilo likitekelezwa, uhuru wa tume ya uchaguzi utavurugwa kwani makamishna watatekeleza majukumu yao kwa misingi ya kisiasa.

Alisema IEBC ingependa sheria iliyopo kwa sasa kuhusu uteuzi wa makamishna ibaki ilivyo, ila marekebisho yanayofaa kufanywa ni kuweka hali ambapo muda wa makamishna kuhudumu utakuwa haukamiliki kwao wote kwa wakati mmoja.

Ijapokuwa ripoti ya BBI ilisema Wakenya wengi walipendekeza uchaguzi ujao usimamiwe na tume mpya, Bw Chebukati alipuuzilia mbali wazo hilo na kusema hiyo ni dhana inayoenezwa na wanasiasa.

Alikosoa jopo la BBI kwa kutotilia maanani chanzo kikuu cha mgawanyiko wa wananchi unaotokea kila wakati wa uchaguzi na badala yake jopo hilo likalaumu tume ya uchaguzi.

“IEBC inahitaji usaidizi kutoka kwa wadau wote ili kuboresha sera zake za kisheria na kiusimamizi ili kutimiza majukumu yake,” akasema.

Alisisitiza kuwa wito wa wanasiasa kutaka kuwe na tume mpya itakayosimamia uchaguzi mkuu ujao ukitekelezwa, kuna hatari ya kuathiri utendakazi wa IEBC kwa kiwango cha kusababisha vurugu za kisiasa.