Raha tele gharama ya kuandaa ugali ikishuka Magharibi
Na BARNABAS BII
WALAJI ugali katika eneo la Magharibi wamepata afueni baada ya bei ya unga wa mahindi kushuka.
Bei zilishuka kufuatia ukosefu wa soko la mahindi kwani kuna bidhaa hiyo tele inayoingizwa nchini kwa bei nafuu kutoka Uganda, wakati ambapo mavuno ya humu nchini pia yamejaa.
Wasagaji mahindi katika eneo hilo jana walisema hawana pa kuuza unga wa mamilioni ya pesa kwa sababu hakuna wanunuzi.
Hii imewalazimu kuteremsha bei hadi Sh90 kwa mfuko wa kilo mbili, kutoka Sh130 miezi miwili iliyopita.
“Tunakumbwa na changamoto kubwa kuuza bidhaa zetu kwa vile wanunuzi ni wachache sokoni ilhali tulitumia fedha nyingi viwandani,” akasema Bw Kipngetich Ngetich kutoka kiwanda cha usagaji mahindi cha Ineet, mjini Eldoret.
Bei ya mahindi ilishuka kutoka Sh3,200 hadi Sh2,800 kwa kila gunia la kilo 90 katika maeneo mengi ya Magharibi baada ya bidhaa hiyo kuwasili kutoka Uganda kwa bei ya chini.
Bidhaa nyinginezo pia zimeanza kushuka bei, kama vile kabeji iliyoshuka hadi Sh1,300 kutoka Sh1,800 na sukuma wiki inayouzwa kwa Sh700 kutoka Sh1,300 kufuatia mavuno tele eneo la Kerio Valley.
“Bei za mahindi zinatarajiwa kushuka zaidi kwa sababu kuna mavuno ya bidhaa mbadala, kuwasili kwa mahindi kutoka Uganda, na mavuno yanayotarajiwa katika eneo hilo,” akasema Bw Moses Kiptoo, mfanyabiashara wa mahindi Eldoret.
Hali hii imetokea wakati ambapo mzozo unatarajiwa kati ya kaunti zilizo chini ya Jumuia ya Kiuchumi Kaskazini mwa Rift Valley (NOREB) na wamiliki wa viwanda vya kibinafsi kuhusu ununuzi wa mahindi kutoka kwa wakulima kupitia kwa madalali.
Kaunti hizo zinataka viwanda vinunue mahindi moja kwa moja kutoka kwa wakulima.