• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 8:55 AM
Maspika wa mabunge ya kaunti wataka kura ya maamuzi mwaka 2022

Maspika wa mabunge ya kaunti wataka kura ya maamuzi mwaka 2022

Na WYCLIFF KIPSANG

MUUNGANO wa Maspika wa Mabunge ya Kaunti (CAF) umeunga mkono mpango wa maridhiano (BBI) lakini unashikilia kuwa ikiwa sharti kura ya maamuzi ifanywe, iwe sambamba na uchaguzi mkuu ujao ili kupunguza gharama.

CAF ambayo ilifanya mkutano wake na mabunge ya kaunti ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Kaskazini mwa Rift Valley (NOREB) katika mkahawa wa Boma Inn, Eldoret ilisema inapendekeza mawaziri wa kaunti wateuliwe miongoni mwa madiwani.

Wanachama wa muungano huo walisema hatua hiyo itapunguza gharama na kuimarisha utoaji hudumu kwa wananchi.

“CAF itayashauri mabunge ya kaunti kuhusu mapendekezo ambayo yanafaa kuwasilishwa kwa jopokazi la BBI. Kati ya mapendekezo mengine, pia tunataka kaunti zipewe uhuru wa kifedha,” akasema Katibu Mkuu wa CAF Kipkurui Chepkwony.

Akaongeza: “Tunaunga mpango wa BBI lakini ikiwa itaendeleza na kuimarisha ugatuzi.”

CAF pia inapendekeza kuanzishwe Mamlaka ya Udumishaji Usalama katika Kaunti (CPA) katika kaunti ambazo zimeathiriwa na kero ya usalama inayosababishwa na uhalifu. Na baadhi ya wanachama wa CPA waketi katika Baraza la Kitaifa la Usalama (NSC).

Mwenyekiti wa CAF James Ndegwa Wahome alisema miradi mingi ya maendeleo imekwama kwa sababu ya utovu wa usalama na kutaka hatua zichukuliwe kukomesha uovu huo.

“Kaunti zinatekeleza wajibu muhimu katika juhudi za kuleta amani na hivyo vinapasa kujumuishwa katika masuala ya usalama. Bila usalama hatuwezi kutarajiwa maendeleo,” akasema Bw Wahome ambaye ni Spika wa Nyandarua.

Kwa miaka mingi, maeneo kadha ya kaunti za Baringo, Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet na Turkana zimekumbwa na utovu wa usalama ambapo mamia ya watu wamepoteza maisha. Hali hiyo imeathiri mipango ya maendeleo katika maeneo hayo.

You can share this post!

Kampuni ya kusambaza maji Mombasa yapinga madai ya...

Mataifa 16 kushiriki katika michuano ya CHAN 2020

adminleo