• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:25 PM
Matiang’i azimwa kufukuza Wachina waliochapa raia wa Kenya viboko

Matiang’i azimwa kufukuza Wachina waliochapa raia wa Kenya viboko

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu Jumatano ilisitisha agizo la Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i lililotaka raia wanne wa China, ambao walinaswa katika video wakimchapa Mkenya, warudishwe kwao.

Jaji Luka Kimaru alisimamisha kutekelezwa kwa agizo hilo la Dkt Matiang’i hadi kesi waliyowasilisha kupinga kutimuliwa isikizwe na kuamuliwa.

Wakili Abdulhakim Abdullahi aliyewasilisha kesi kwa niaba ya Deng Hailan, Ou Qiang, Yu Ling na Chang Yueping, alieleza mahakama kwamba Dkt Matiang’i aliamuru washukiwa hao warudishwe kwao kinyume cha agizo la mahakama kuwa wazuiliwe seli kwa siku 15.

Wakili huyo alimsihi Jaji Kimaru awazuie polisi kuwaondoa rumande washukiwa hao na kuwasafirisha hadi China.

Mahakama ilifahamishwa kuwa haki za washukiwa hao zitakuwa zimekiukwa endapo watasafirishwa makwao kabla ya uchunguzi kukamilishwa.

Jaji Kimaru aliamuru afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na ile ya Mwanasheria Mkuu zikabidhiwe nakala za kesi hiyo ndipo wawasilishe ushahidi.

Mahakama iliombwa iwape washukiwa hao wanne muda wa kujitetea na kueleza sababu za kuendelea kukaa nchini.

“Polisi wanahitaji muda kurekodi taarifa kutoka kwa mwathiriwa ambaye inadaiwa alifukuzwa kazi baada ya kupata kichapo kwa kufika kazini akiwa amechelewa,” alisema hakimu.

Mahakama ilisema mlalamishi huyo alisafiri kutoka Nairobi hadi mashambani kwa vile hakuwa na njia ya kujikimu kimaisha baada ya kutimuliwa kazini na mwajiri wake.

Wakiwasilisha ombi la kutaka washukiwa hao wazuiliwe, vongozi wa mashtaka Jacinta Nyamosi na Everlyn Onuga walieleza korti kuwa inahofiwa washukiwa watatoroka endapo wataachiliwa kwa dhamana.

Mahakama ilielezwa kuwa Polisi watawasiliana na Idara nyingine za Serikali kama vile Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA) kubaini ikiwa wanne hao walikuwa wanalipa kodi kutokana na ajira yao.

Polisi walisema hati za Idara ya Uhamiaji walizokuwa nazo wanne hao zilionyesha walikuwa wameingia nchini kama watalii na hawana vibali vya kufanya kazi nchini.

You can share this post!

Kalonzo ageuza wimbo, asema hataki Waziri Mkuu mwenye...

Sonko alilia mahakama itupe kesi dhidi yake

adminleo