• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
Gavana aahidi watoto maziwa kila siku katiba ikibadilishwa

Gavana aahidi watoto maziwa kila siku katiba ikibadilishwa

Na Gitonga Marete

SERIKALI ya Kaunti ya Meru imetumia zaidi ya Sh100 milioni kwa mpango wa kununulia watoto wa chekechea maziwa.

Kiwango hicho cha fedha kimetumiwa tangu mpango huo ulipoanzishwa miaka miwili iliyopita. Gavana wa Meru, Bw Kiraitu Murungi alisema mpango huo ambao ulianza Februari 2018 umesaidia sana kuongeza idadi ya watoto wanaojiunga na shule za chekechea katika kaunti nzima.

Alisema endapo katiba itabadilishwa na kuongeza fedha kwa serikali za kaunti, utawala wake utahakikisha watoto wanapewa maziwa kila siku badala ya mara mbili kwa wiki ilivyo sasa.

“Hadi sasa, tumetumia Sh145 milioni kununulia watoto wetu maziwa kupitia kwa mpango huo na tuna matumaini ya kuendelea kama tutapata fedha zaidi,” akasema.

Bw Murungi aliomba bunge la kaunti lihakikishe bajeti ya maziwa ya watoto haitapunguzwa katika mwaka wa fedha wa 2020/2021.

Alikuwa akizungumza wakati wa kuzindua upya mpango wa kulisha watoto wa shule katika Shule ya Msingi ya Gitoro mnamo Jumanne.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo maafisa wa Chama cha Ushirika cha Uzalishaji Maziwa Meru.

 

You can share this post!

Kiambu yateua Naibu Gavana mpya

Echesa achunguzwe alivyoingia kwa ofisi yangu – Ruto

adminleo