Habari

Thiwasco yaimarisha huduma ya usambazaji maji Thika

February 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya Maji ya Thiwasco Water Company Ltd imeweka mikakati ya kuboresha huduma kwa wateja.

Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Bw Moses Kinya, alisema tayari wameanza kufanya mabadiliko ya kuweka mabomba ya kusambaza maji ili kutosheleza mahitaji ya wateja wao.

“Tumeanza kuweka mabomba mapana ya kusambaza maji maeneo tofauti na kuhakikisha tunaongeza kiwango cha maji tunayosambaza kwa wateja. Pia wateja wetu wameongezeka kwa wingi kwa kipindi cha miaka michache tu ambayo imepita,” alisema Bw Kinya.

Alitaja maeneo ya Githunguri, Landless, na Witeithie kama zile zilizoongezeka na wakaaji na kwa hivyo usambazaji wa maji lazima uongezeke.

Alisema kampuni ya Thiwasco ndiyo inayotambulika kama inayosambaza maji kwa njia ya kisasa kote nchini, baada ya kupata kibali maalum cha ISO 9001-2015.

Mkurugenzi wa Thiwasco Water Company Ltd Bw Moses Kinya akihutubia washikadau waliohudhuria mkutano wa kila mwaka. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema kampuni hiyo inasambaza maji mjini Thika na maeneo ya karibu ambapo wateja ni zaidi ya 300,000.

Alisema bado wanapitia changamoto za hapa na pale kwa sababu wanakosa ardhi ya kutosha ya kupanua mipango yao ya kusambaza maji kwingineko.

“Iwapo tutapata kipande cha ardhi cha kutosha bila shaka tutaweza kusambaza maji maeneo mengine na wateja wetu wataongezeka kwa wingi,” alisema Bw Kinya.

Alisema maeneo mengine ambayo anatarajia kuongeza mabomba ya maji ni Makongeni na Kiganjo mjini Thika kutokana na ongezeko la idadi ya watu.

“Kulingana na ukuaji wa teknolojia ya kisasa ni sharti hata sisi tufuate mkondo huo ili tuhudumie wateja wetu kwa njia ifaayo,” alisema mkurugenzi huyo.

Waziri wa Maji na Mazingira katika Kaunti ya Kiambu, Bw David Kuria alipongeza juhudi zinazofanywa na kampuni ya Thiwasco za kusambaza maji kwa wakazi wa Thika kwa jumla.

Alipendekeza kuwe na mpango wa kuhifadhi maji kwa wingi hasa wakati kuna mvua nyingi ili maji hayo yaweze kunufaisha watu wakati wa kiangazi.

“Ni jambo la busara kuhifadhi maji ili kusiwe na upungufu wowote. Maji ni uhai na kwa hivyo si vyema kuwa na upungufu ilhali maji mengi hupotea bure wakati wa mvua,” alisema Bw Kuria.

Alisema visima pia ni muhimu katika makazi ili wakati wowote ule kusiwe na shida ya maji kukiwa na ukame.

Naye Bw John Mwangi alisema kampuni ya Thiwasco imekuwa mstari wa mbele kusambaza maji kwa wakazi wa Thika kwa miaka mingi na kwa hivyo ni vyema kufanya kazi nao kwa ushirikiano wa karibu.

“Cha muhimu ni kuhakikisha watu wanaonyakua vipande vya ardhi wanakabiliwa vilivyo kwa sababu Thiwasco imeshindwa kujipanua kwa sababu hakuna kipande cha ardhi cha kutosha,” alisema Bw Mwangi.

Madiwani (MCAs), waliohudhuria hafla hiyo walisema watafanya juhudi kuona ya kwamba kampuni hiyo inafanikiwa katika juhudi zake za kusambazia wateja maji mjini Thika na hata Kiambu kwa jumla.

Bw Lawrence Kamangathi alisema gavana Bw James Nyoro amejitolea kuona ya kwamba anafanya kazi kwa ushirikiano na kampuni ya Thiwasco ili wakazi wa Kaunti ya Kiambu wapate maji ya kutosha.