'Wanafunzi Wuhan hawatasafirishwa kuja nchini'
Na DIANA MUTHEU
SERIKALI haijaweka mikakati yoyote kuwaondoa Wakenya kutoka China; taifa ambalo limeathirika pakubwa ma virusi vya Corona.
Msemaji wa serikali, Cyrus Oguna, akizungumza na wanahabari katika majengo ya GPO Posta, Nairobi alisema Alhamisi kuwa serikali imetuma Sh1.3 milioni zigawanywe miongoni mwa wanafunzi 91 na wanasarakasi tisa walio mjini Wuhan ambapo virusi hivi viliripotiwa kwa mara ya kwanza.
“Pia, tumetuma pesa zingine ambazo kupitia ubalozi wetu huko China wataweza kupata mahitaji ya kila siku,” alisema Bw Oguna.
Bw Oguna aliwaomba wazazi wa wanafunzi hao wasiwe na hofu kwani hakuna hata mmoja wao ameambukizwa homa hiyo ambayo wataalamu sasa wanaita Covid-19.
“Wako salama. Wanaishi katika vitongoji tofauti na tunahofia katika mchakato wa kuwakutanisha katika sehemu moja ili wasafirishwe kuja nchini, huenda wakaambukizwa. Ni heri watulie tukiendelea kuwapa msaada,” alisema.
Mkurugenzi wa Idara ya Afya katika Wizara ya Afya Dkt Patrick Amonth alisema wamejiandaa kupambana na virusi vya corona.
“Tuna vifaa 5,000 vya kuziba pua na mdomo, tumeongeza idadi ya wahudumu wa afya katika uwanja wa ndege, bandari na mipaka. Ni lazima kila mtu anayeingia nchini apimwe. Pia, ni vizuri wananchi wadumishe usafi na pia wapige ripoti kuhusu mtu yeyote wanayemshuku kuwa na dalili ya virusi hivi,” akasema Dkt Amoth.