• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
NHIF yahitaji mageuzi ili kuboresha afya – Kagwe

NHIF yahitaji mageuzi ili kuboresha afya – Kagwe

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Seneta wa Nyeri Mutahi Kagwe aliyeteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa Waziri wa Afya amesema Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) inahitaji kufanyiwa mageuzi makubwa ili iwezeshe serikali kufikia lengo la Afya kwa Wote (UHC).

Bw Kagwe alisema hazina hiyo haipasi kuendeshwa kama kampuni yenye lengo la kuchuma faida kupitia michango ya wanachama bali inafaa kutumia pesa inazokusanya kugharamia matibabu ya wananchi moja kwa moja.

Aliwaambia wabunge waliokuwa wakimchunguza kubaini ufaafu wake wa wadhifa wa Waziri wa Afya kwamba ilikuwa makosa kwa sheria ya NHIF kufanyiwa mbadiliko na kuipa jukumu la kuendesha shughuli zake kama kampuni ya kutoa huduma za bima.

“Mheshimwa Spika NHIF inapasa kutoa huduma kwa wananchi na wala haipasi kuonekana kana kwamba inaendesha shughuli za bima kwa minaji ya kupata faida. Hii ni kwa sababu hazina hii haina wataalamu katika nyanja ya utoaji bima,” akasema Bw Kagwe.

Aliongeza kuwa ipo haja ya Bodi ya NHIF pia inapasa kuteua Afisa Mkuu Mtendaji mpya ili kutoa uongozi kwa asasi hiyo.

Bw Kagwe alikuwa akijibu swali kutola kwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi Spika Justin Muturi ambaye alitaka kujua hatua ambayo atachukua kuhakikisha kuwa takriban Sh6 bilioni ambazo NHIF imeweka katika akaunti mbalimbali za benki zinatumiwa kuendeleza wajibu wake.

Aidha, Bw Muturi alitaka kujua zinazopelekwa faida zinazozalishwa na fedha hizo ambazo zinanuiwa kufadhili huduma za afya.

“Pesa ambazo NHIF hukusanya kutoka kwa wananchi zikianza kufanyiwa biashara, hazina hii itakosa kuwa na manufaa kwa wananchi inavyopasa,” Muturi akasema.

Katika siku za hivi karibuni hazina hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kifedha hali iliyoipelekea kuanzisha masharti makali kwa wanachama wake. Na wasimamizi wake wamekuwa wakikabiliwa na shutuma za ufisadi.

Kwa mfano, ilitoa adhabu ya kima cha asilimia 50 kwa wale ambao watakosa kuwasilisha michango yao ya kila mwezi. Hata hivyo, masharti hayo yalisimamishwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Vile vile, Bw Kagwe aliitaka serikali kuelekeza pesa zote inazolipwa kwa kampuni za bima kwa NHIF ili iweze kuwa na fedha za kutosha kuiwezesha kukadiria kiwango cha michango ambayo wanachama wanapaswa kutoa

Aliongeza kuwa ipo haja ya Bodi ya NHIF pia inapasa kuteua Afisa Mkuu Mtendaji mpya ili kutoa uongozi kwa asasi hiyo.

Wakati huu hazina hiyo inaendeshwa na Nicholas Odongo kama kaimu afisa mkuu tangu 2018 Bw Geoffrey Mwangi alipofutwa kazi kwa kuhusishwa na sakata ya ufisadi ya kima cha Sh2 bilioni.

You can share this post!

NCIC yanguruma hofu ikitanda kuhusu mkutano wa BBI

Polisi anayelinda ofisi ya Ruto apatikana amefariki

adminleo