Habari Mseto

Tangatanga wasusia hafla ya BBI Narok, Ruto akifokea Raila

February 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

ALEX NJERU na GEORGE SAYAGIE

WANASIASA wanaoegemea mrengo wa Tangatanga Jumamosi walisusia mkutano wa kupigia debe Mpango wa Maridhiano (BBI) katika Kaunti ya Narok ulioongozwa na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga.

Hii ni licha yao kuahidi kwamba wangehudhuria mikutano hiyo maeneo mbalimbali nchini. Lakini hali ilikuwa tofauti Jumamosi kwani wanasiasa hao, wanaomuunga mkono Naibu Rais, Dkt William Ruto, hawakuonekana kwenye mkutano huo.

Baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakihudhuria mikutano hiyo ni Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Bw Kipchumba Murkomen, Kiranja wa Seneti, Bi Susan Kihika, wabunge Moses Kuria (Gatundu Kusini), Kimani Ichung’wa (Kikuyu) miongoni mwa wengine.

Hii pia ni kinyume na awali ambapo walihudhuria mikutano iliyoandaliwa katika miji ya Mombasa na Kitui. Hata hivyo, viongozi hao walijipata pabaya katika Kaunti ya Kitui, wakati Bw Kuria aliposhambuliwa na wananchi wenye ghadhabu.

Kwenye mkutano wa Jumamosi, viongozi wanaomuunga mkono Dkt Ruto katika Kaunti ya Narok pia walitimiza ahadi waliyotoa Ijumaa kwa kuususia.

Viongozi hao ni mbunge wa Emurrua Dikiir, Bw Johanna Ng’eno, Naibu Gavana wa Narok, Bi Everlyn Aruasa, madiwani Jefferson Lang’at (Ololung’a), Bw Wesley Koech (Sagamian), Bw Sammy Kositany (Ailmootiok), Bw Philemon Aruasa (Melelo) na Bw Gabriel Mibei (Angata Barikoi).

Viongozi hao walilalamika kwamba viongozi wa jamii ya Maasai walikuwa wakiwatenga viongozi wa jamii tofauti.

“Hatutahudhuria mkutano ambao unaendeshwa kwa kuzitenga baadhi ya jamii za eneo hili,” alisema Bw Ng’eno.

Dkt Ruto alizuru kaunti za Tharaka Nithi na Laikipia, ambako alimkashifu vikali Bw Odinga kwa kuwaongoza wanasiasa wa ODM kuchochea jamii mbalimbali nchini, kwa kisingizio cha kupigia debe BBI.

Akihutubu kwenye hafla ya kuchangisha fedha katika Kanisa Katoliki la Tunyai, eneobunge la Tharaka, Dkt Ruto alisema kuwa lengo kuu la wanasiasa wa ODM ni kuigawanya nchi kwa misingi ya kikabila, ili kuhakikisha kuwa baadhi ya jamii hazipati nafasi ya uongozi.

Alisema kuwa mipango hiyo ni hatari, kwani inaweza kuzua mapigano nchini, ikiwa haitakomeshwa.

“Ningetaka kuwaambia viongozi wa ODM ambao wanaeneza chuki za kikabila miongoni mwa jamii mbalimbali kwamba mwenendo kama huo umepitwa na wakati. Nikiwa Naibu  Rais wa Kenya, mimi na Rais Uhuru Kenyatta, hatutaruhusu mambo hayo kuendelea, kwa kisingizio cha kupigia debe BBI,” alisema.

Dkt Ruto alisema kuwa ni dhahiri kwamba “dhoruba ya Tsunami” aliyokuwa akiirejelea Odinga na washirika wake ni njama ya kubagua baadhi ya jamii kwenye uongozi wa nchi.

“Kila Mkenya ana haki ya kufanya kazi, kuishi na kutafuta uongozi katika sehemu yoyote ile nchini bila kujali jamii anayotoka,” alisema.