• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:10 PM
Mzungu alia kutapeliwa na mwanamke Mkenya

Mzungu alia kutapeliwa na mwanamke Mkenya

Na BRIAN OCHARO

RAIA mwanamume wa Uingereza amelalamikia jinsi mwanamke Mkenya alivyomfilisi na kumwacha fukara.

Kupitia kesi iliyowasilishwa mahakamani, imefichuka Bw Kevin Donald Binnie alikuja kutalii Kenya mwaka wa 2010 alipokutana na Bi Phyllis Wairimu Jamin ambaye baadaye alimperemba na kumwacha akiwa maskini wa kutupwa.

Mapenzi baina ya wawili hao yalianzia mtandaoni kabla ya Binnie kuja Kenya na wawili hao wakaishi pamoja.

Mapenzi yao yalikolea na ilipofika Januari 1, 2011, walioana rasmi na kuhamia eneo la Gilgil.

Bw Binnie alirejea nyumbani Uingereza na kuuza mali yake na kisha kusafirisha iliyosalia nchini Kenya ili kuanza maisha mapya na mkewe.

Baada ya kuuza mali, alituma fedha katika akaunti ya benki ya Bi Wairimu ili anunue kipande cha ardhi ya kujenga nyumba yao ambapo wangeishi.

Bi Wairimu alimwambia kuwa ardhi hiyo isajiliwe kwa jina lake kwa kuwa Mwingereza huyo alikuwa raia wa kigeni wala hakuwa na nambari ya mlipa ushuru kutoka kwa Mamlaka ya Ushuru (KRA).

Walinunua ardhi kwa Sh1.3 milioni na kisha wakaongezea magari kadhaa, wakajenga nyumba ya vyumba vitatu vya kulala na kidimbwi cha kuogelea.

Hata hivyo, miezi michache baada ya kuhamia katika nyumba hiyo, wawili hao walikosana na kutengana Julai 2012 kutokana na mizozo ya mara kwa mara.

Baada ya kurejea nchini Uingereza kujiliwaza, Mwingereza huyo anasema kuwa alishtuka kuona mitandaoni Bi Wairumu akitafuta wateja wa kununua nyumba yake.

Mawakili wake walimthibitishia kuwa kweli Bi Wairimu alikuwa akitafuta wateja wa kununua nyumba hiyo.

Mwingereza huyo alienda kortini kusimamisha uuzaji wa nyumba yake lakini kufikia wakati wa kuwasilisha kesi kortini, Bi Wairimu alikuwa ameuza nyumba hiyo kwa Sh6.5 milioni kwa Bi Teresia Murugi Murigi.

Mzungu huyo amelalamika kwamba, nyumba haikuuzwa kwa njia ya haki kwani alihitajika kutoa ruhusa kama mumewe Bi Wairimu.

Bi Wairimu amepinga madai hayo akisema mzungu huyo hakuwa mume wake kwani alimwacha alipomtendea uzinifu.

Katika uamuzi wake uliotolewa Septemba 29, 2016, Jaji Mary Kasango, alitoa agizo la kusimamisha uuazaji wa nyumba hiyo.

Korti ilimrejeshea Binnie umiliki wa nyumba hiyo lakini hawezi kuishi ndani kwani imeharibiwa na baadhi ya vifaa kuondolewa.

Wakati huo huo, Bi Murigi sasa amemshtaki Bi Wairimu katika Mahakama ya Ardhi na Mazingira baada ya kugundua kuwa alimuuzia mali ya utapeli.

Mwingereza huyo alitoa taarifa za benki kortini kuthibitisha kwamba alinunua shamba, magari na kujenga nyumba hiyo kwa fedha zake bila usaidizi kutoka kwa mkewe.

You can share this post!

TAHARIRI: Idadi ya watu isizidi maendeleo ya nchi

Awaka demu kuzidisha bili ya mlo

adminleo