• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Sumu Ya Bafe: Kazi inayoukosoa uongozi mbaya kijazanda

Sumu Ya Bafe: Kazi inayoukosoa uongozi mbaya kijazanda

Jina la utungo: Sumu ya Bafe

Mwandishi: K.W. Wamitila

Mchapishaji: Vide-Muwa

Mhakiki: Nyariki Nyariki

Kitabu: Tamthilia

Kurasa: 75

Bafe ni jazanda ya ukoloni mkongwe na ukoloni mambo leo. Pazia linapofunguka, inashuhudiwa sherehe ya ndovu kumla mwanawe inayoongozwa na Mheshimiwa Mapepe, kiongozi wa Dahimu. Anawahimiza wananchi kucheza kwa furaha kwa kufuata midundo ya nyatiti, kilumi, siwa na ala nyingine za kitamaduni.

Kinachosherehekewa hapa ni mazishi ya bafe. Wepesi wa kufahamu mambo kama vile Mwapinduzi hawana budi kuung’amua unafiki wa viongozi wanaoongoza sherehe ya kumzika bafe. Mwapinduzi anapasua jipu:

‘‘ Yule nyoka aitwaye bafe hajafa bado!’’

Kauli hii inakuwa sumu ya bafe katika moyo wa Mheshimiwa Mapepe ambaye anamkaripia, kumtisha na kumwonya vikali Mwapinduzi. Babu Bakongwe anapomwuliza Mwapinduzi iwapo kweli bafe amezikwa, jibu la Mwapinduzi linakuwa la shaka.

Mwapinduzi: Ndiyo, wanasema wamemzika.

Bakongwe: Huamini wewe Mwapinduzi?

Mwapinduzi: Kusema kweli Babu Bakongwe, nina hofu…

Hofu ya Mwapinduzi inathibitika wazi baadaye akina Mapepe wanapoongozwa na utashi wao na kusahau jukumu muhimu walilokabidhiwa. Wanyonge wanafutwa kazi kwa kisingizio cha kubana matumizi.

Hii inatokea hivyo kwa kuitikia masharti ya wafadhili ili kupewa mkopo. Wafanyakazi hao wanyonge wanaanzisha magenge ya kujikimu ila magenge yenyewe yanabomolewa kwa kisingizio cha kuusafisha mji ili kuwavutia watalii.

Pesa zinavujwa kwa mambo yasiyo muhimu kama vile kulipia ziara za aila ya Mapepe kwenda kujiburudisha ughaibuni na katika ujenzi wa mnara wa kumkumbuka Mapepe.

Akina Babu Bakongwe waliojitolea mhanga kumwinda ‘bafe’porini wanasahauliwa na badala yake kupokwa ardhi ili kujenga mnara. Tentan-Belwa, barakala wa Mapepe anatunga nyimbo za kuwapumbaza wananchi kwamba mambo yangali sawa.

Mmoja kati ya nyimbo hizo na ambao unaimbwa kote katika vyombo vya habari unahusu ‘kutokomezwa’ kwa bafe. Wananchi wanafanywa kuamini kuwa bafe hayuko tena miongoni mwao inavyodaiwa na ‘maadui’.

Kupitia kwa mabarakala wa Mapepe, wananchi wanafanywa kuamini kuwa matatizo yaliyowakabili ni ya ulimwengu mzima hivyo basi wanapaswa kujikaza viuno.

Hatima ya uongozi mbaya inakuwa ni maandamano ya wananchi, jambo linalomsukuma Mapepe kutoka uongozini.

Babu-Mzuka anawakanya wananchi kuwa ni mapema mno kusherehekea kupinduliwa kwa uongozi wa Mapepe kwani bado wangalipo bafe wengine waliobaki miongoni mwao na watakaohitaji kukabiliana nao kwa muda mrefu.

Matumizi ya jazanda na tashtiti yanatawala msuko wa tamthilia nzima.

You can share this post!

Mradi wa NiE ni lulu inayowaniwa Shuleni Sangenyi, Taita...

NYARIKI: Kuomba radhi kwa kutohudhuria mkutano ni udhuru,...

adminleo