Sonko amkabidhi Uhuru usimamizi wa Nairobi
Na WAANDISHI WETU
GAVANA Mike Sonko wa Nairobi Jumanne alikabidhi usimamizi wa huduma za jiji kwa serikali kuu.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Ikulu Kanze Dena, hatua hiyo iliafikiwa kwenye mkataba uliowekwa sahihi jana kati ya Bw Sonko na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa.
Bi Dena alisema makubaliano hayo yaliungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta na uwekaji sahihi ulishuhudiwa na Spika Kenneth Lusaka wa Seneti na Mwanasheria Mkuu Paul Kihara.
Makubaliano hayo yanaipatia serikali kuu usimamizi wa huduma muhimu zikiwemo afya, uchukuzi, ujenzi, mipango na maendeleo.
Huduma za jiji zimetatizika chini ya uongozi wa Bw Sonko, hali ambayo imezorota tangu alipokatazwa na korti kufika ofisini mwake baada ya kushtakiwa kwa wizi wa mali ya umma.
Pia Bw Sonko anakabiliwa na mswada katika bunge la kaunti unaolenga kumwondoa madarakani.
Kwingineko, Gavana wa Meru Kiraitu Murungi, amewaonya viongozi wa mrengo wa Tangatanga dhidi ya kuvuruga mkutano wa Jopokazi la Maridhiano (BBI), utakaoandaliwa uwanja wa Kinoru hapo Jumamosi.
Bw Murungi aliwashauri viongozi hao wasithubutu kufika uwanjani na kuzua taharuki akisema eneo hilo halina historia ya vurugu na halitaki kuachwa nyuma kwenye mchakato wa BBI.
“Mwelekeo utakaotolewa kuhusu BBI katika uwanja wa Kinoru ni wa Mlima Kenya na si wa kaunti au viongozi wenyewe. Hatutaki watu ambao wataleta ubabe wa kisiasa wakati wa mkutano huo,” akasema Bw Murungi.
“Nimewasikia baadhi ya watu wakisema mikutano ya BBI ni ya kupoteza wakati. Iwapo wewe ni moja wao, basi nakuomba usifike Kinoru bali usalie nyumbani badala ya kupoteza wakati wako bure,” akaongeza.
Alisema hayo jana baada ya kukutana na Kinara wa ODM Raila Odinga pamoja na magavana wengine wa Mlima Kenya.
Wakati wa kikao hicho, viongozi hao walitangaza kwamba maandalizi yote kuhusu mkutano huo yamekamilika.
Zaidi ya watu 30,000 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wa BBI ambao utashirikisha kaunti 10 zinazounda Muungano wa kiuchumi wa Mlima Kenya.
Bw Murungi pia alithibitisha kwamba Bw Odinga atakuwa mgeni wa heshima ingawa pia wametuma mwaliko kwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye bado hajathibitisha iwapo atafika.
Gavana wa Nyandarua Francis Kimemia, Anne Waiguru wa Kirinyaga, Ndiritu Mureithi wa Laikipia na Muthomi Njuki wa Tharaka-Nithi ni miongoni mwa viongozi wengine waliohudhuria kikao cha jana.
Mkutano huo ni kwenye msururu wa ile imekuwa ikifanyika maeneo mbalimbali ya nchi kupigia debe BBI.
Ripoti za Collins Omulo, Erick Matara na Hamisi Ngowa