HabariSiasa

Kelele za siasa Kenya coronavirus ikibisha

February 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na WAANDISHI WETU

MAAMBUKIZI ya coronavirus yameingia hatua hatari yakisambaa nje ya China kwa kasi zaidi kuliko ndani ya nchi hiyo ambako yalizuka Desemba 2019.

Pia wasiwasi umezuka kufuatia watu ambao hawajatangamana na wagonjwa kugunduliwa wanaugua homa hiyo.

Kulingana na gazeti la New York Times la Marekani, maradhi hayo yaliingia hatua ya kutisha Alhamisi maafisa wa afya wa Amerika na Ujerumani walipogundua kuna maambukizi ya watu wawili ambao hawajatangamana na walio na virusi hivyo.

Maafisa walisema hii imezua uwezekano kuwa virusi hivyo vimeanza kusambaa vyenyewe, hali inayotarajiwa kufanya iwe vigumu kujua chanzo chake na kuwatenga wanaoshukiwa kuugua.

WHO ilisema maambukizi nje ya China yameongezeka kufuatia kuenea kwa virusi hiyo hasa nchini Italia, Korea Kusini na Iran.

Maradhi hayo sasa yamesambaa katika mabara yote baada ya Algeria kuripoti kisa barani Afrika huku kingine kikitokea Brazil katika Amerika Kusini.

Makamu wa rais wa Iran Masoumeh Ebtekar na mwenyekiti wa kamati ya kigeni bungeni Majotaba Zolnour wameripotiwa kuambukizwa

Kufuatia tahadhari hiyo ya WHO, mataifa mengi duniani yamechukua tahadhari.

Nchini Amerika, Rais Donald Trump amemteua makamu wake Mike Pence kuongoza kamati ya kupambana na janga hilo.

Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe naye jana aliagiza shule zote kufungwa kwa muda usiojulikana kuzuia usambaaji wa maradhi hayo.

Mataifa mengine nayo yametangaza hatua ambazo zitachukuliwa kuzuia kuingia kwa watu walioambukizwa na pia mbinu za kufuatwa iwapo visa vyovyote vitagunduliwa.

MAPUUZA KENYA

Lakini hali ni tofauti hapa Kenya ambapo viongozi wakuu wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga, pamoja na wafuasi wao, wameweka taifa katika hali ya uchaguzi mkuu kwa siasa za ubinafsi, huku wakipuuza hatari ya coronavirus.

Dkt Ruto na Bw Odinga wanamezea mate urais katika uchaguzi wa 2022 na kila mmoja amekuwa akiwaongoza wafuasi wake kujipigia debe na kudhalalisha mwenzake.

Mivutano ya Dkt Ruto na Bw Odinga pia imetawala mchakato wa maridhiano (BBI) kiasi kwamba taifa limetekwa kwenye siasa zao za ubinafsi huku masuala muhimu kama coronavirus, nzige, hali ngumu ya uchumi, uhaba wa nafasi za kazi, vita dhidi ya ufisadi miongoni mwa mengine yakisahaulika.

Viongozi hao wanatumia muda wao mwingi kurushiana cheche za maneno kwenye mikutano, mazishi, makanisani, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kiasi cha kusahau dharura ya coronavirus.

Lakini wanasiasa hao wakuu hawajasikika wakizungumzia suala la janga la coronavirus.

Cha kutamausha ni kuwa licha ya kubainika kuwa coronavirus imesambaa zaidi nchini China ilikozuka Desemba, serikali imekuwa ikiruhusu ndege zinazotoka nchini humo kuleta watu hapa Kenya bila hatua mwafaka za kuhakikisha maradhi hayo hayapenyi nchini.

Katika uchunguzi wa Taifa Leo katika vituo vya afya hapa nchini, baadhi ya wahudumu walikiri kuwa hata hawajui coronavirus ni nini.

Wengine walisema hawajapewa mafunzo yoyote na serikali kuhusu jinsi ya kutambua virusi hivyo na pia hakuna vifaa walivyopewa vya kupima.

Katika uwanja wa ndege wa JKIA kumekuwepo na uchunguzi wa kukagua joto la mwili lakini hakuna mikakati ya kufuatilia wale ambao huenda wameambukizwa lakini hawajafika hatua ya kuonyesha dalili.

Ubalozi wa China nchini umekuwa ukiwataka raia wake wanaoingia nchini kujitenga kwa siku. Lakini raia wa mataifa mengine wanaokuja kutoka China hawawekewi masharti kama hayo.

Mnamo Jumatano, abiria 239 waliosafiri Kenya kwa ndege kutoka China waliruhusiwa nchini lakini Wizara ya Afya ikawashauri wajitenge kwa siku 14.

Hapo Alhamisi, Ubalozi wa Uchina nchini ulithibitisha kwamba shirika la ndege la China Southern Airlines limerejelea safari zake kutoka Guangzhou hadi Nairobi.

Taarifa kutoka Ubalozi huo zilisema Wizara ya Afya nchini ilikuwa imearifiwa mapema, na kwamba abiria wote waliokuwa katika ndege hiyo walikuwa wamefanyiwa uchunguzi wa kiafya na kushauriwa wajitenge kwa kipindi cha siku 14 baada ya kufika hapa Kenya.

Wananchi waliohojiwa na Taifa Leo wameeleza wasiwasi wa janga iwapo virusi hivyo vitaingia nchini kutokana na ukosefu wa maandalizi ya kukabiliana na maradhi hayo.