Referenda haiwezekani Julai – Karua
Na BENSON MATHEKA
KIONGOZI wa chama cha Narc Kenya, Martha Karua, amepuuza kauli ya kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwamba Kenya itafanya kura ya maamuzi Julai 2020.
Bi Karua alisema kwamba Bw Odinga anadaganya Wakenya kwa sababu katiba inatoa utaratibu wa kufuatwa kabla ya kura ya maamuzi.
“Ni ndoto isiyoweza kutimia kuamini kwamba kura ya maamuzi itafanyika Julai 2020 ilhali kuna utaratibu wa kikatiba ambao ni lazima ufuatwe. Tusidaganye Wakenya,” Bi Karua alisema kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi.
Bi Karua aliwataka Wakenya kukataa kulazimishwa kuunga ripoti ambayo hawaielewi au wanayozimwa kujadili na kushiriki kikamilifu.
Bw Odinga na wabunge wa chama chake cha ODM wamekuwa wakisema kuwa mchakato wa BBI utakamilika Julai kwa kura ya maamuzi ya kubadilisha Katiba.
Ijumaa, Bi Karua alitilia shaka lengo halisi la mikutano ya kujadili ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), akisema inaharakishwa ilhali Wakenya hawajaisoma na kuielewa.
“Inashangaza mpango huu unavyoharakishwa bila kuwapa Wakenya fursa ya kusoma ripoti yenyewe. Inashangaza kwamba miezi mitatu tangu kuzinduliwa kwa ripoti hiyo Wakenya hawajapewa nakala wajisomee,” alieleza.
Aidha, alikosoa jinsi mikutano hiyo inavyoendeshwa akisema baadhi ya wanasiasa wanaitumia kutoa matamshi ya chuki.
“Mikutano inayofanyika kabla ya mikutano ya hadhara ya uhamasisho inahudhuriwa na wale wanaoalikwa pekee. Hii inafungia nje Wakenya wengi ambao ndio wanapaswa kutoa maoni ikiwa mchakato huu unahusu maslahi ya Wakenya,” alisema.
Kulingana na Bi Karua ni viongozi wanaounga BBI pekee wanaoalikwa kuhudhuria mikutano hiyo ilhali inapaswa kupitisha maazimio ya wakazi wote.
Alisema kila Mkenya ana haki ya kushiriki katika mpango huo hata kama haungi mkono yanayopendekezwa.
Baadhi ya wanasiasa hasa wanaounga Naibu Rais William Ruto wamekuwa wakilalamika kuwa maoni yao yamekuwa yakipuuzwa katika mikutano ya kimaeneo ya BBI.