• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
WATOTO: Japo walemavu, wamedhihirisha umahiri wao katika uigizaji na densi

WATOTO: Japo walemavu, wamedhihirisha umahiri wao katika uigizaji na densi

Na PATRICK KILAVUKA

Kweli ulemavu si hali ya kukosa uwezo kutekeleza majukumu au wajibu katika nyanja mbalimbali za maisha.

Kauli hii imedhihirika peupe baada ya wanafunzi taahira kutoka shule ya St Catherine Mentally Handicap, Butula, Kaunti ya Busia kuwika kwenye mashindano ya Kitaifa ya Tamasha za Drama ambazo zilifanyika shule ya upili ya Lenena, Kaunti ya Nairobi.

Walionesha ueledi wa kutumia vipaji vyao vya kuigiza, kuimba na kusakata densi kwa njia maridadi sana hadi wakulaza sakafuni shule zenye uwezo.

Huu ulikuwa mwaka wa tatu mtawalia na wamehifadhi taji hilo la densi bunifu ya kitamaduni baada ya kutawazwa mabingwa wa kitaifa katika kategoria hiyo.
Wamelibeba taji hilo mwaka 2016, 2017 na 2018 na hivyo basi wataliweka daima.

Mwaka huu, walikuwa na wasilisho la densi yenye dibaji ya Omukeka ambalo lilikuwa na maana fiche kuhusu wizi wa mtihani chini ya mtayarishi na msimamizi mkuu wa shule Gladys Orlendo.

Wanafunzi wa shule ya St Catherine Mentally Handicap, Butula, Kaunti ya Busia wakishiriki mashindano ya kitaifa ya tamasha za drama yaliyoandaliwa shule ya Lenena, Kaunti ya Nairobi. Picha/Patrick Kilavuka

Wasilisho hilo lilionesha bayana jinsi vishawishi vya ufisadi vinasababisha tendo hilo ovu kutendeka.

Linakariri kwamba utepeli wa mtihani unatokana na walimu kutokuwa kuwa na mbinu kabambe za ufukunzi, kutokuwajibika kwa wanafunzi na walimu, kutokamilisha mtaala ipasavyo na kuzembea katika ufunzaji kunapekelea wanafunzi ambao hawakutayarishwa vyema kuibiwa mtihani ili kuwe na matokeo bora.

Changamoto hiyo ya njia mbadala na ya mkato katika kupita mtihani kwa kufunika ukweli kulinda jina na hadhi ya shue ndiyo inataswiriwa kama Omukeka (Zulia).

Isitoshe, linakariri pia ukosefu wa vifaa vya masomo shuleni kuchangia pia.

Kulingana na jopo la ukaguzi, shule hii ndiyo ilibuka na wasilisho bora la densi bunifu ya kiasili, uelekezi, utunzi, uelekezi wa ishara, ulimbwende na jezi bora, uchezaji ala bora na utayarishi mufti chini ya mtayarishi na msimamizi mkuu wa shule Orlendo.

Kwa usakataji wa densi, hauwawezi. Picha/Patrick Kilavuka

Zaidi ya hayo, walitoa bingwa wa kinadada na wanaume wa kitaifa wa densi bunifu ya  kitamaduni. Frederick Otieno(huongoza nyimbo na anasomea sayansi ya masuala ya nyumbani shuleni) alitawaza kuwa mwanadensi bora kitengo cha wanaume ilhali upande wa kinadada, Nelly Kundu,12, ( kiongozi wa nyimbo na shule, ambaye anajifunza ushonaji na ususi) alitawazwa mahiri.

Wote walipokea vyeti kuwa viongozi bora katika densi hiyo ambayo iliibuka kuwa bora kitengo hicho.

Kabla kufika katika mashindano ya kitaifa, wasanii hawa ishirini na watano, walikuwa wamehemesha shule zingine kuanzia kaunti ya Butula ambapo wasilisho lao lilikuwa kidedea katika mashindano yaliyofanyiwa shule ya upili ya Bukhalarire.

Waliendelezi kampeni yao kwa kuibuka kileleni mwa Kaunti ya Busia ambapo patashika lilifanyiwa shule ya upili ya Budalangi High. Hatimaye, walisonga mbele kutetea ubingwa wao katika ya Kanda ya Magharibi katika mashindano  yaliyoandaliwa shule ya Upili  ya Vihiga na kuwa bingwa tena.

Wanafunzi wa shule ya St Catherine Mentally Handicap, Butula, Kaunti ya Busia waonyesha vyeti na mataji waliyozoa katika mashindano ya kitaifa ya tamasha za drama yaliyoandaliwa shule ya Lenena, Kaunti ya Nairobi.Picha/Patrick Kilavuka

Siri ya ufanisi?  Licha ya changamoto kuwepo, wanajiamini na wanajua kwamba, wanatalanta bora, usaidizi wa hali na mali kutoka kwa usimamizi wa shule, wanadensi kufurahia usanii wao, kutumia wakati wao vyema na uwajibikaji wa walimu pamoja na kuamini kwamba kupitia maombi, Mola atawafanikishe.

Ushauri wa wanavipaji hawa na mwalimu mkuu kwa wazazi ni kwamba, watoto walemavu wana uwezo sawa na wale wengine na hawafai kufichwa! Ila, wapewe fursa ya kuangaza na kutumia utajiri wa vipawa vyao vya masomo na masuala ya anwai na watahisi kana kwamba, hawabaguliwi katika jamii na taifa na watakuwa wenye furaha.

Isitoshe, serikali izikumbatie shule hizi na usaidizi wa vifaa na kuwalipia wanafunzi karo. Pamoja na hayo, walazimu wazazi kuwasomesha watoto hao, kuwapa malezi bora, wawazingatie na kupewa kipa umbele.

Mwisho shule inashukuru kampuni ya rununu ya Safaricom kwa kuinunulia basi na ufadhili wa mpango wa maendeleo ya makuzi ya maeneo wa Butula (CDF) na serikali kwa kuikumbatia na kuifaa na udhamini.

You can share this post!

Wenye ardhi wataka wafidiwe

Familia ya Moi iheshimiwe, viongozi waionya Jubilee

adminleo