MCAs wa ODM kukutana kujadili hatima ya Sonko
Na COLLINS OMULO
MADIWANI wa Chama cha ODM katika Kaunti ya Nairobi wamepanga kukutana kujadili kama wataunga mkono kutimuliwa kwa Gavana Mike Sonko.
Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kaunti, Bw David Mberia alifichua kwamba Kiongozi wa ODM Raila Odinga alikuwa ameshauriana na Rais Uhuru Kenyatta aliyekutana na baadhi ya madiwani Ikuluni kuwashauri wasiendeleze mpango wa kumtimua Sonko.
“Nafahamu kuwa mkutano wa Ikulu uliandaliwa ifaavyo na kwa ushauriano baina ya kiongozi wa chama Raila Odinga lakini bado nasubiri kufahamishwa yaliyoamuliwa.” akasema Bw Mberia.
“Tutaandaa mkutano na wanachama wenzangu kujadili mkondo tutakaochukua lakini hakuna hakikisho kuwa mswada (wa kumbandua) hautawasilishwa siku za usoni,” akaendelea.
Alisema hivyo hata wakati wenzake walikuwa wakishikilia kuwa wataendelea kuuwasilisha mswada huo na kupiga kura kumbandua Bw Sonko, japo kuna waliosema watatii ombi la Rais Kenyatta na kutounga mkono ubanduaji wa Bw Sonko.
Kiranja wa wachache katika bunge la kaunti hiyo Peter Imwatok amesema bado atawasilisha hoja ya kumtimua Sonko mbele ya bunge.
Bw Imwatok hakuhudhuria kikao cha ikulu na alisema kuwa nia yake ni kupigana na ufisadi na ukosefu wa maadili, na hivyo kuingiliwa kisiasa hakutazima lengo lake.
Diwani wa Embakasi Michael Ogada naye alisema ataunga mkono hoja hiyo, akisema japo Rais aliingilia kati hali ambayo huenda ikaathiri jinsi kura zitapigwa, kamwe yeye hangekubali kulazimishwa kufanya jambo.
“Sijiungi na waliokubali kulazimishwa kutoendelea. Sielewi kwa nini Rais anasema anakabiliana na ufisadi tena anatetea mtu fisadi,” akasema Bw Ogada.
MCA wa Woodley Mwangi Njihia pia alisema ataunga mkono hoja hiyo.