Echesa aendelea kuandamwa na madai ya uhalifu
Na MARY WAMBUI
ALIYEKUWA Waziri wa Michezo Rashid Echesa, ameendelea kuandamwa na masaibu baada ya maafisa kutoka Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) Jumatatu kuvamia nyumbani kwake katika mtaa wa Karen, Nairobi na kumkamata kwa madai ya kuhusika katika uhalifu.
Maafisa hao walilazimika kuingia katika boma lake kwa nguvu mwendo wa saa tano asubuhi, baada ya kuzuiwa kuingia.
Katika harakati hizo, walifanya msako na wakaishia kuondoka na nakala na magari matano; ambayo ni Mercedes Benz KCL 350J, V8 KCW 298Q, Lexus KBY 750U, Volkswagen KAY 388A na Pick-up KBPV 725B.
Kulingana na afisa aliyeongoza msako huo, Bw Ahmed Abdikadir, msako huo ulichochewa na uchunguzi unaoendelea kuhusiana na madai ya kuchukua magari ya Bi Esther Kabura kwa njia zisizo halali.
Bi Kabura, katika nakala za kiapo, alidai kuwa marehemu mumewe Patrick Akifuma ambaye alifariki Machi 14, 2016, alikuwa rafikiye Bw Echesa na kuwa wawili hao walikuwa pamoja siku ambayo alifariki.
Bi Kabura pia aliambia maafisa wa DCI kuwa waziri huyo wa zamani alikuwa na mazoea ya kukodisha gari aina ya Toyota Landcruiser V8 KBZ 009J kutoka kwa mumewe na kuwa hadi wakati wa kufariki kwa mumewe, Bw Echesa alikuwa amelikodisha na hakuwa amerejesha.
Alisema kuwa alijaribu kumwitisha Bw Echesa gari hilo bila mafanikio, lakini baadaye akagundua kuwa waziri huyo wa zamani alikuwa amebadili usajili wake pamoja na mengine mawili; Toyota Mark X KBN 242W na Passat KAY 388A, kuwa yake na kwa njia ya ulaghai.
“Afisa wa uchunguzi atahitajika kufanya msako katika makazi yake, nyumbani na afisi ili kubaini madai na kutafuta ushahidi,” Bw Abdikadir akasema katika nakala za kiapo.
Baada ya takriban saa tano za msako wa kutafuta magari yaliyokuwa yameegeshwa katika boma la Bw Echesa jana, maafisa wa uchunguzi waliyaweka mafuta na kuyaendesha hadi Makao Makuu ya DCI, wakienda na Bw Echesa kumhoji.
Wakili wake, aliyekuwa hakimu Kiambu, Bw Brian Khaemba alisema kuwa suala hilo liliibuliwa kwa mara ya kwanza wakati Bw Echesa alikuwa akipigwa msasa bungeni, baada ya kuteuliwa kuwa waziri.
“Bunge lilipokeza DCI suala hilo kwa uchunguzi na baada ya uchunguzi kukamilika, kiongozi wa idara ya kuzuia uhalifu hatari DCI akaandikia bunge akisema waziri huyo wa zamani alikuwa amenunua gari lenyewe kihalali na hivyo hakufanya uhalifu wowote,” Bw Khaemba akasema.
Alisema kuwa ilishangaza jinsi suala lenyewe lilirejeshwa kutoka DCI, ofisi ambayo ilimwondolea lawama Bw Echesa.
“Unakaa kuwa uchunguzi wa uhalifu lakini kuna mambo mengi ambayo hayahusiani na utafutaji wa haki. Nakala zote za umiliki wa magari pamoja na magari matano yamechukuliwa, ilhali mlalamishi aliibua tetesi kuhusu gari moja. Kwa jumla, DCI imezuilia magari sita ya mteja wangu, la sita lilizuiliwa Februari alipokamatwa katika kesi nyingine,” akasema.
Aliongeza kuwa mmoja wa wanawe Bi Kabura aliandikia DCI barua akisema kuwa mamake alimuuzia Bw Echesa gari husika.
Bw Echesa tayari anakabiliwa na kesi mahakamani ambapo yeye pamoja na washukiwa wengine watatu wamekana mashtaka yanayohusiana na ulaghai wa Sh39 bilioni.