• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 4:25 PM
Mkutano wa BBI Eldoret wafutwa

Mkutano wa BBI Eldoret wafutwa

ERIC MATARA na ONYANGO K’ONYANGO

MKUTANO wa kuupigia debe Mpango wa Maridhiano (BBI), ambao ulikuwa umeratibiwa kufanyika mjini Eldoret baadaye mwezi huu, uliahirishwa Jumanne kwa hofu ya usalama.

Mkutano huo ulikuwa umepangwa kufanyika Machi 21. Ulikuwa umepangwa na kundi la kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, linalojumuisha viongozi wanaounga mkono muafaka kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.

Kundi hilo linapinga mrengo wa ‘Tangatanga’ unaowajumuisha wanasiasa wanaounga mkono mpango wa Naibu Rais William Ruto kuwania urais mwaka wa 2022.

Tashwishi za kuandaa mkutano huo mjini Eldoret zilianza kujitokeza baada ya jumbe za vitisho kuanza kusambazwa.

Gavana Lee Kinyanjui wa Nakuru alieleza kuwa baada ya mashauriano na mwenzake Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet), walikubali kufutilia mbali mkutano huo.

Bw Kinyanjui ndiye mshirikishi mkuu wa mpango huo katika eneo la Bonde la Ufa Kusini huku Bw Tolgos akiwa mshirikishi wake eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Badala yake, viongozi hao walikubali kuandaa mkutano wa pamoja katika uwanja wa Afraha, Nakuru siku iyo hiyo.

“Tulikuwa tumepanga mkutano wa Eldoret kufanyika hapo Machi 21. Hata hivyo, baada ya kushauriana mnamo Jumatatu jioni, tulikubali kufanya mkutano wa pamoja mjini Nakuru.

“Kwa sasa, hakutakuwa na mkutano wowote wa BBI mjini Eldoret, lakini watu wengine wanaweza kupanga kufanya mkutano wao kuko huko,” akasema Bw Kinyanjui kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Bw Tolgos pia alitoa kauli kama hiyo.

Na ijapokuwa viongozi hao walishikilia kuwa walichukua hatua hiyo ili kutoa nafasi kwa mashauriano zaidi kuhusu ripoti hiyo, ilibainika kuwa mkutano wa Eldoret ulifutiliwa mbali kwa hofu ya kuzuka kwa ghasia.

Duru ziliiambia Taifa Leo kwamba hilo ndilo lilichangia waandalizi kubadilisha mahali ambapo mkutano huo ungefanyika.

“Kulikuwa na ripoti kwamba ghasia zingetokea. Waandalizi walichagua Nakuru, ikizingatiwa kuwa ni eneo ambalo jamii mbalimbali zinaishi. Ingekuwa vigumu sana kwa Bw Odinga kuhutubu kwenye mkutano wa Eldoret,” zikaeleza duru.

Eldoret ni ngome ya kisiasa ya Dkt Ruto, ambaye pia ni mkosoaji mkubwa wa Bw Odinga.

Hata hivyo, Bw Tolgos alipuuzilia mbali madai hayo, akishikilia kwamba washirika wa Dkt Ruto pia wako huru kuandaa mkutano wao.

Alisema kuwa kila mmoja amekaribishwa kuhudhuria mkutano wa Nakuru, ingawa aliwaonya washirika hao kutozua mafarakano yoyote.

“Tumekuwa tukiliambia kundi la ‘Tangatanga’ kuwa ikiwa halitaki kuhudhuria mikutano yetu, basi linapaswa kuandaa mikutano yake ambayo hatutahudhuria. Vilevile, tunawakaribisha katika mikutano yetu ijapokuwa lazima waheshimu taratibu zilizotumika kuiandaa,” akasema Bw Tolgos.

Alisema kuwa katika mkutano wa Nakuru, watabuni mapendekezo ambayo yatakabidhiwa wenyeji wa Eldoret kwenye mkutano mwingine ambao utafanyika mahali tofauti.

Magavana hao wawili waliteuliwa na Rais Kenyatta kuendesha mipango ya mikutano hiyo katika maeneo ya Kusini na Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Bw Kinyanjui alisema kuwa mkutano wa Nakuru utaziunganisha kaunti 10 kutoka eneo hilo.

You can share this post!

WAFALME! Man-City wabeba kombe kwa mara ya 3 mfululizo

Mfanyabiashara Nginyo Kariuki azikwa Tigoni

adminleo