MKU yaweka mkakati mpya wa kuboresha shughuli na utoaji huduma
Na LAWRENCE ONGARO
KUNA haja ya kila mfanyakazi kuzingatia majukumu aliyopewa kuyatekeleza ili kufanikisha malengo ya mwajiri wake.
Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kimebuni mpango mpya utakaofuatwa na kila mdau ili kufuatilia jinsi kila mfanyakazi anavyotekeleza wajibu wake.
Kila mfanyakazi atalazimika kutia saini mkataba wa utendaji kazi kwa lengo la kufuatilia kwa makini jinsi kazi inavyoendshwa chuoni.
Mwenyekiti wa kamati ya chuo hicho Profesa David Serem, alizindua mwelekeo mpya utakaofuatwa wa utendaji kazi wa kila mfanyakazi ili kufanikisha mahitaji muhimu yanayoendeshwa na chuo hicho.
Alisema mpango huo ulibuniwa mwaka wa 2012, lakini ulikuwa kwa maafisa wa ngazi ya juu pekee, lakini wameona ni muhimu uheshimiwe na kila mmoja ili kuendesha chuo hicho kwa njia inayostahili.
“Baada ya bodi kuu ya maafisa wa Chuo kuketi chini, waliona ni vyema pia kuwahusisha wafanyakazi wote ili kila mfanyakazi ajulikane ni kazi ipi anayofanya na jinsi anavyoiendesha,” alisema Prof Serem.
Alisema kamati yake iliketi chini na kuafikia uamuzi huo aliosema ni wa kuridhisha na kutia moyo, huku akidai ni hatua ya kupongezwa na wote.
Aliyasema hayo mnamo Jumatatu katika ukumbi wa chuo hicho alipowahutubia wahadhiri, wanafunzi na wafanyakazi wa chuo hicho.
Alisema hatua hiyo inamaanisha kuwa kila mfanyakazi atalazimika kutia saini mkataba maalum kukubali ya kwamba atafanya kazi kwa njia inayostahili bila kuhujumu kazi hiyo.
“Nina matumaini ya kwamba mpango huo utabadilisha mwelekeo wa kazi katika chuo hiki na kila mfanyakazi atajituma kufanya kazi yake kwa bidii. Kwa hivyo ninatumai kila mmoja anaelewa ni kwa nini ametia saini mkataba huo,” akasema Prof Serem.
Alisema mpango wa ruwaza wa chuo hicho wa mwaka wa 2015 hadi 2019 ulikamilika Desemba 2019 na kwa hivyo wanalenga pia kuendeleza ruwaza ya 2020 hadi 2029 kwa lengo la kupiga hatua zaidi.