Kaunti kujenga kiwanda cha kusafisha asali
Na Samuel Baya
SERIKALI ya Kaunti ya Nakuru imepanga kutumia Sh5 milioni kujenga kiwanda cha kusafisha asali katika kaunti hiyo.
Waziri wa kilimo katika kaunti hiyo, Dkt Immaculate Maina alisema shughuli za kiwanda hicho zitasimamiwa na Chama cha Ushirika cha Makinanjo ambacho kinapatikana katika eneo hilo.
“Mpango wetu ni kuhakikisha kuwa wafugaji wa nyuki katika chama hicho wananufaika,” akasema.
Alisema kiwanda hicho kitajengwa kwa awamu kadhaa kuanzia kwa kutafuta mkandarasi ambaye ataendeleza zoezi hilo. Kulingana na waziri huyo, Nakuru ina zaidi ya mizinga 100,000 ya nyuki lakini takribani asilimia 40 ya mizinga hiyo haina nyuki kwa sasa.
Alisema kaunti imeanzisha utafiti wa asali yote inayovunwa katika eneo hilo ili kutathimi ubora wake kwani inaaminika kuna asali ghushi katika baadhi ya maduka.
Utafiti huo unatekelezwa na watafiti kutoka chuo kikuu cha Egerton na taasisi ya utafiti ya uzalishaji wa nyuki iliyoko jijini Nairobi.
Vilevile, utafiti huo utatambua hali ya ubora wa asali kwani imesemekana wafugaji wengine hutumia mbinu hatari kusafisha asali yao.