SHAIRI: Buriani Matiba, ulazwe pema peponi

Na KULEI SEREM

Nimetingwa na huzuni, nimepokea habari,
Inanichoma moyoni, kama moto msumari,
Shujaa wetu jamani, ametuaga kwaheri,
Ni buriani Matiba, ulazwe pema peponi.

Wakenya twaomboleza, kwa hakika tunalia,
Nimekuwa nikiwaza, ukweli taka kujua,
Habari zikaeleza, ya kwamba aliugua,
Ni buriani Matiba, ulazwe pema peponi.

Ni wa vyama vingi baba, alitengeneza njia,
Kaumia awe tiba, kuleta demokrasia,
Jasiri yule Matiba, sasa ametangulia,
Ni buriani Matiba, ulazwe pema peponi.

Kama cha puani chuma, alikuwa ni imara,
Kidete alisimama, akatuonyesha dira,
Aliziongoza vyema, alizoshika wizara,
Ni buriani Matiba, ulazwe pema peponi.

Wakati wa uwaziri, kaleta mabadiliko,
Alikuwa ni jasiri, tena mwenye ongezeko,
Licha kuwa mashuhuri, kapata masikitiko,
Ni buriani Matiba, ulazwe pema peponi.

Mateso ya gerezani, na wale watu watesi,
Alitiwa mikononi, bila kustahili kesi,
Aliumia kichwani, kapatwa na kiharusi,
Ni buriani Matiba, ulazwe pema peponi.

Kwaheri wetu jagina, makiwa! Kwa familia,
Sijui ila Rabana, yeye mwenyewe ajua,
Mioyoni lako jina, daima litabakia,
Ni buriani Matiba, ulazwe pema peponi.

Habari zinazohusiana na hii

Comments

 • adminleo

  01/14/2019

  1. Hawalipwi, wao hujitolea kuandika.
  2. Shairi hutumwa kwa baruapepe taifa@ke.nationmedia.com
  3. Ubora wa shairi, uzito wa ujumbe, uzingativu wa kanununi za utunzi/arudhi (shairi liwe tarbia – beti tano)
  4. Kwa kununua gazeti kila Jumamosi na Jumapili
  5. Ndio – Wengi wanaochangia kwa sasa ni Watanzania

  Shukran,

  Taifa Leo Dijitali.

 • Ali Mohammed

  01/11/2019

  Habari,

  Nimekuwa kwa muda mrefu nikifuatilia gazeti lenu kwa njia ya mtandao, hususan katika sehemu inayohusu Mashairi, hii nikutokana binafsi ni mpenzi wa mashairi na vilevile najaribu kutunga mashairi, ningependa kujuwa yafuatayo:

  1. Hawa washairi ambao mnachapisha mashairi yao huwa wanalipwa? na ni kiasi gani?
  2. Jee! ni njia ipi hutumika kuwasilisha mashairi kwenu?
  3. Ni vigezo gani, hutumika hadi shairi la mshairi likaikia kushinda na hadi kuwekwa katika gazeti lenu?
  4. taarifa humfika vipi mshairi kama shairi lake limechapishwa katika toleo fulani la gazeti
  5. Jee! mtanzania anaweza kutuma mashairi kwenu na kupata fursa kama hizo?

  Ahsante
  Ali Mohammed (Almar)
  Zanzibar

Leave a Reply