Habari MsetoSiasa

Igathe njiani kwa cheo chake cha naibu gavana?

March 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA JOSEPH WANGUI

UTATA wa uongozi ambao umekumba Kaunti ya Nairobi kwa muda mrefu sasa umechukua mwelekeo mpya baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufichua kwamba, haikupokea barua kuhusu kujiuzulu kwa Polycarp Igathe kama Naibu Gavana.

IEBC ilikuwa ikijibu barua ya Karani wa Bunge la kaunti na Spika Beatrice Elachi waliotaka ushauri kuhusu uongozi wa Nairobi. Ilifichua kwamba, haijawahi kupata barua ya Bw Igathe ambaye alijiuzulu 2018.

“Kuhusiana na pengo la uongozi katika afisi ya Naibu Gavana wa Kaunti ya Nairobi, tume bado haijapokea barua yoyote rasmi ila tu ilisikia habari hizo kupitia vyombo vya habari,” ikasema barua ya IEBC.

Barua ya IEBC ilitiwa saini na Mkurugenzi wa Masuala ya Kisheria, Michael Goa Januari 9, 2020. Bw Goa alikuwa akijibu kaunti kwa niaba ya Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, Hussein Marjan.

Bi Elachi na karani wa kaunti waliandikia tume hiyo, kupitia wakili John Diro baada ya uamuzi wa mahakama kumzuia Gavana Mike Sonko kuingia afisini kutokana na kesi za ufisadi zilizokuwa zikimkabili.

Aidha, wawili hao pia waliwasilisha ombi katika Mahakama ya Juu wakitaka kufahamu mwelekeo wa kuendesha jiji kutokana na masaibu yanayomkumba Bw Sonko.

Barua ya IEBC sasa inadhihirisha kwamba, kujiuzulu kwa Bw Igathe hakujawahi kuchapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali na ni ishara kwamba, Bw Sonko hawezi kumteua mtu wa kurithi nafasi hiyo.

Bw Igathe aliondoka afisini 2018 baada ya kukosa kuelewana na magavana kuhusu majukumu mbalimbali ya kaunti.

Kwa mujibu wa IEBC, uteuzi wa Anne Mwenda kama naibu gavana unamaanisha kwamba, Bw Sonko alilenga tu kuwa na manaibu gavana wawili kwa sababu Bw Igathe bado yupo afisini.

Aidha, tume hiyo ilikataa kugusia kuzuiwa kwa Bw Sonko kuingia afisini, ikisema kwamba mahakama ina jukumu la kutoa mwelekeo kuhusu suala hilo.

“Kuhusiana na ushauri wetu kuhusu hali ya sasa ya kaunti na hali ya baadaye, tumebaini kwamba tume haina mamlaka au jukumu la kuhusika na usimamizi wa kila siku wa masuala ya kaunti. Hatuwezi kuzungumzia suala hilo,” akasema Bw Goa.

Spika na karani pia waliwasilisha ombi wakitaka kufahamu iwapo kuna pengo katika afisi ya Bw Sonko na iwapo alikuwa na mamlaka ya kumchagua naibu wake. Vilevile walitaka kufahamu iwapo Spika anaweza kuwa kaimu gavana mwenye mamlaka kulingana na sheria.

Maombi yao jana yaliwasilishwa kwenye Mahakama ya Juu ili kesi hiyo itajwe na Naibu Msajili Ole Keiwua ambaye alisema Mwenyekiti wa IEBC, Mwanasheria Mkuu na Serikali ya Kaunti hawakuwa wamewasilisha utetezi wao.

Bw Keiwua alitaka pande zote ziwasilishe utetezi wao ndani ya siku saba kisha Jaji Mkuu David Maraga ateue jopo la majaji wa kusikiza kesi hiyo.