• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Msajili vyama atoa onyo kali kwa usitishaji wa uchaguzi

Msajili vyama atoa onyo kali kwa usitishaji wa uchaguzi

Na JUSTUS OCHIENG

VYAMA vikuu vya kisiasa nchini, kikiwemo chama tawala cha Jubilee, vinakabiliwa na hatari ya kufutiliwa mbali ikiwa havitaendesha chaguzi zao inavyohitajika kisheria.

Vyama hivyo ni pamoja na ODM kinachoongozwa na Raila Odinga, Wiper cha Bw Kalonzo Musyoka na ANC kinachoongozwa na Musalia Mudavadi.

Vingine ni Ford Kenya na Kanu vinavyoongozwa na Moses Wetang’ula na Gideon Moi, mtawalia.

Kutokana na mgawanyiko ndani ya chama cha Jubilee kati ya mirengo ya Tangatanga na Kieleweke, mng’ang’ano umeibuka kati ya wafuasi wa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, kila upande ukipania kudhibiti chama hicho.

Jubilee ilipanga kufanya uchaguzi mashinani na kitaifa mwezi huu wa Machi lakini mkutano wa kujenga muafaka kuhusu shughuli hiyo haujafanyika.

ODM imeahirisha uchaguzi ili kutoa nafasi kwa mchakato unaoendelea wa kufanikisha Mpango wa Maridhiano (BBI). Kufikia sasa, hamna wagombeaji ambao wametangaza viti wanavyopanga kuwania katika ODM.

Lakini katika Jubilee, kiranja wa wengi Benjamin Washiali ametangaza nia ya kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa kitaifa huku mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria akisema anapania kutwaa kile cha katibu mkuu kinachoshikiliwa na Bw Raphael Tuju.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu aliambia ‘Taifa Jumapili’ katika mahojiano kwamba kuna haja ya vyama vyote vilivyosajiliwa kufanya uchaguzi kama njia ya kutimiza matakwa ya kisheria.

“Chama kizuri sharti kiandae uchaguzi kila mara kulingana na kipengee 91 cha Katiba,” akasema.

Bi Nderitu alisema uchaguzi huwa suala la ndani ya vyama, akiongeza kuwa endapo kuna changamoto zozote zilizopelekea vyama kukosa kuandaa chaguzi, “sharti vitoe sababu maalum na vitoe makataa mapya.”

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna alielezea imani kwamba chama hicho kitaandaa uchaguzi mwaka huu.

Naye naibu mwenyekiti wa Wiper Mutula Kilonzo Junior alisema chama hicho kitaanda uchaguzi baada ya mchakato wa BBI kukamilishwa.

“Hata hivyo, msajili wa vyama anapaswa kutoa fedha kwa vyama ili viweze kufadhili shughuli muhimu kama hizi,” Bw Kilonzo akasema. Katibu Mkuu wa ANC, Barack Muluka alisema matayarisho ya uchaguzi yameanza huku mwenzake wa Ford Kenya, Dkt Eseli Simiyu akisema wamekamilisha uchaguzi mashinani na wameanza mipango ya kuandaa uchaguzi wa kitaifa.

“Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (ADC) la chama chetu litafanyika mwishoni mwa Machi ili kushughulikia masuala mbalimbali ya chama,” Dkt Simiyu akasema.

Naye Katibu Mkuu wa Kanu, Bw Nick Salat alisema ni muhimu kwa vyama kuandaa uchaguzi kwani hiyo ndiyo njia ya “kubaini vyama halisi na vile vya ‘mikoba”.

“Tunamshukuru Msajili wa Vyama vya Kisiasa kwa kuhimiza uwepo wa uthabiti katika vyama. Tayari tumetimiza hitaji la kijinsia na lile la watu wanaoishi na ulemavu. Sasa tunalenga kuhakikisha kuwa tumefanya chaguzi zetu mwaka huu,” akasema Bw Salat.

You can share this post!

DINI: Tumia thawabu yako kama mama kuwalea watoto wako kwa...

BBI yafufua mjadala wa siasa za majimbo Pwani

adminleo