• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
ODM yatisha kumng’oa Dkt Ruto

ODM yatisha kumng’oa Dkt Ruto

DICKENS WASONGA na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine viongozi ODM wamedokeza kuwa huenda wakadhamini hoja ya kumng’oa mamlakani Naibu Rais William Ruto wakisema uchunguzi unaoendeshwa dhidi ya afisi yake ni dhihirisho baadhi ya mambo yameshusha hadhi ya asasi ya urais.

Seneta wa Siaya James Orengo ndiye alitoa dokezo hilo Jumamosi aliposema chama hicho kinapanga kutumia njia za kikatiba kuadhibu Naibu Rais.

“Baada ya muda wa wiki mbili tutaanzisha mchakato wa kumwadhibu,” akasema Orengo katika eneobunge la Bondo, Kaunti ya Siaya wakati wa halfa ya mazishi ya Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) Profesa Gilbert Ogutu.

Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga na kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi.

Wanasiasa hao wa ODM pia waliendelea kumshinikiza Dkt Ruto aseme ‘ukweli’ kuhusu kifo cha Sajini Kipyegon Kenei ambaye alikuwa Mkuu wa Ulinzi Afisini mwake katika Jumba la Harambee House Annex, Nairobi.

Viongozi hao walikuwa; Dkt Gedion Ochanda (Bondo), Elisha Odhiambo (Gem), Opiyo Wandayi (Ugunja) Jacklyn Oduol (Mbunge Maalum), Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Siaya Dkt Christine Ombaka na Dkt Oburu Oginga wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Wengine walikwa ni Otiende Amolo (Rarieda) na magavana Peter Anyang’ Nyong’o (Kisumu) na mwenzake wa Siaya Cornel Rasanga.

Wanasiasa hao walimtaka Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti kumchunguza Dkt Ruto, kutokana na sababu kwamba amekuwa akizungumzia uchunguzi huo hadharani na mitandaoni.

Kulingana na kipengee cha 150 (b) cha Katiba, Naibu Rais anaweza kuondolewa mamlakani akikiuka Katiba au sheria nyingine, ikiwa kuna sababu tosha za kuaminika kuwa ametenda uhalifu unaokiuka sheria za kitaifa na kimataifa, au kutokana na mienendo mibaya.

Hoja ya kumwondoa afisini Naibu Rais sharti iungwe mkono na angalau thuluthi mbili ya wajumbe katika bunge la kitaifa na lile la seneti.

Wakati huu Dkt Ruto anaungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge na maseneta, ishara kwamba huenda ikawa vigumu kwa hoja ya kumwondoa mamlakani kupita.

Aidha, wadadisi wanasema kuwa Rais Uhuru Kenyatta hawezi kuruhusu hoja kama hiyo kuwasilishwa bungeni kwa sababu itachafua hewa ya kisiasa nchini na kuvuruga mchakato unaoendelea wa maridhiano (BBI).

“Nadhani Orengo na wenzake wanatoa vitisho tu. Wakati huu mandhari ya kisiasa sio faafu kwa hoja kama hiyo. Rais Kenyatta na Bw Odinga hawawezi kuikubali kwani itavuruga mpango wao wa BBI,” anasema Bw Martin Andati.

You can share this post!

BBI yafufua mjadala wa siasa za majimbo Pwani

Harambee Starlets yafundishwa soka na Chile kwa kupigwa 5-0

adminleo