Habari Mseto

Kanisa Katoliki laonya kuhusu kikundi potovu Nairobi

March 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na NDUNGU GACHANE

KANISA Katoliki jijini Nairobi limeonya kuhusu kikundi haramu ambacho kinashinikiza umma kukumbatia tamaduni potovu zilizo hatari kama vile ukeketaji wa wanawake na dhuluma za wanawake.

Kupitia arafa iliyotumwa na Kadinali John Njue kwa makanisa yote ya Katoliki, kanisa hilo lilieleza wasiwasi kwamba kikundi hicho kinachojiita Gwata Ndai kinalazimisha waumini wa kanisa hilo kujiunga nalo.

Kulingana na Kanisa Katoliki, kikundi hicho kina kila ishara za dhehebu potovu litakaloathiri vibaya watu na kuvunja familia, kanisa na jamii kwa jumla.

Arafa hiyo iliyosomwa makanisani Nairobi na Kiambu, ilifichua kwamba kikundi hicho kina makao yake makuu katika maeneo ya Kiambaa, Githunguri, Lari, Limuru, Ikinu, Githurai 44 na Mai Mahiu, katika Kaunti ya Kiambu, na maeneo mbalimbali Nairobi.

Askofu Njue alisema athari za kikundi hicho zimefanya baadhi ya waumini kuhama kanisa hilo.

“Kikundi hicho kinatumia mbinu ya vitisho kutafuta wafuasi na kulazimisha watu kukifuata. Kumekuwa na ripoti zilizowasilishwa kwetu kuhusu familia nyingi zilizovunjika, vita na matatizo ya kiakili hasa kwa wanawake na watoto,” Kadinali Njue akasema.

Katika mahojiano kwa njia ya simu, Kadinali Njue alisema waliarifiwa kuhusu kikundi hicho mwezi uliopita wakati wa mkutano wa baraza la kanisa hilo.

Alisema kwamba wakati huo, alimwagiza Kasisi Emmanuel Ngugi kuongoza kamati ambayo ilitoa ripoti iliyothibitisha kweli kikundi hicho kipo.

“Nilibuni kamati ambayo ilifanya uchunguzi ikatoa ripoti kuhusu makundi ambayo yanaeneza kurudishwa kwa mbinu za kale za maombi na vilevile kukitisha mizizi tamaduni potovu za kale,” akasema katika mahojiano.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki aliomba waumini wa kanisa hilo washikilie mafunzo na maadili ya dini kikamilifu pamoja na maadili mema ya kijamii, akiongeza kwamba kuna njia ambazo Wakristo wanaweza kutumia kutekeleza mahitaji ya kitamaduni bila kuasi dini.

Alitaka waumini wajiepushe na hatari ya kuchanganya mafunzo ya dini na itikadi za kitamaduni ambazo hazistahili katika jamii ya sasa.

Kadinali Njue aliagiza makasisi kutafuta waumini waliopotoshwa ambao wangependa warudishwe kanisani kwa kufuata mwongozo wa kanisa ambao unajumuisha kufunga na kuomba faraghani.

“Kwa wale ambao huenda mlipotoshwa na mafunzo ya makundi aina hiyo, ningependa kuwakaribisha upya kanisani,” akasema.