Msijaribu kuvuruga BBI Afraha, Tolgos aonya Tangatanga
Na ONYANGO K’ONYANGO
GAVANA wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos, amewaonya viongozi wa mrengo wa Tangatanga dhidi ya kuvuruga au kuteka ratiba ya mkutano wa Jopokazi la Maridhiano (BBI) unaotarajiwa kuandaliwa uga wa Afraha Jumamosi.
Bw Tolgos pia amewaonya viongozi hao ambao ni wandani wa Naibu Rais Dkt William Ruto dhidi ya kuwakosea heshima Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga iwapo watakabidhiwa nafasi ya kuhutubu siku hiyo.
Hata hivyo, aliwaalika viongozi wote kwenye mkutano huo utakoshirikisha magatuzi yote ya Kaskazini na Kati mwa Bonde la Ufa baada ya mkutano uliopangiwa kufanyika katika uwanja wa 64 jijini Eldoret kufutiliwa mbali wiki iliyopita.
“Wale ambao wamekuwa wakipinga BBI na hatimaye wameona nuru, wapo huru kujiunga nasi. Hata hivyo, lazima waheshimu Rais na Bw Odinga ili tuamini kwamba wamebadilika.
“Lazima wafahamu kwamba hawawezi kuteka mkutano ambao tumeandaa kwa muda mrefu kisha kuuvuruga. Lazima wakunje mkia na kufuata ratiba yetu,” akasema Bw Tolgos.
Gavana huyo ambaye ni mwandani wa Seneta wa Baringo Gideon Moi, aliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuongoza kampeni za BBI katika ukanda wa Bonde la Ufa.
Hata hivyo, amekuwa na wakati mgumu kuwaunganisha viongozi wa eneo hilo ambao wapo kwenye mirengo ya Dkt Ruto na wale wanaomuunga mkono Bw Moi pamoja na Bw Odinga.
Aidha Bw Tolgos akizungumza na Taifa Leo, alifichua kwamba amekuwa akiandaa mazungumzo na viongozi ambao wameonyesha nia nzuri kusaidia kupanga mkutano wa Jumamosi.
“Tumekuwa tukishauriana na kuweka mikakati yote kuhakikisha mkutano wetu unafana. Hii itahakikisha kwamba kauli itakayotolewa kwa niaba ya kaunti zetu inajumuisha maoni ya wote. Baada ya mkutano wa Afraha, tutakuwa tukiandaa mikutano mengine ya BBI maeneo tofauti bondeni,” akaongeza Bw Tolgos.
Hata hivyo, nyufa zimeanza kuonekana baada ya baadhi ya viongozi kudai watahudhuria mkutano huo tu iwapo watapokezwa ruhusa na Dkt Ruto. Walipinga kufutiliwa mbali kwa mkutano wa Eldoret, wakisema Bw Tolgos na kundi lake waliogopa kuonyeshwa kivumbi na mrengo wa Tangatanga.
“Hatupingi mkutano huo ila tunasubiri mwelekeo kutoka kwa jenerali wetu. Hata hivyo, ni wazi waliogopa kufika Eldoret kutokana na hofu ya kuzomewa na raia kwa sababu wamekuwa wakimdharau Naibu Rais,” akasema Mbunge wa Keiyo Kusini, Bw Daniel Rono.
Mbunge wa Belgut, Bw Nelson Koech naye alizua maswali kuhusu mkutano kati ya Bw Odinga na viongozi wengine wiki jana, akisema mirengo yote haikuwakilishwa.
Waliokutana na Bw Odinga wiki jana ni wabunge Joshua Kutuny (Cherangany), Silas Tiren (Moiben), William Kapket (Tiaty), Bw Tolgos miongoni mwa viongozi wengine.
“Hata kama tutahudhuria, kuandaliwa kwa mkutano huo kumekuwa siri mno na hatujahusishwa,” akasema Bw Koech.
Baada ya mkutano wa Afraha, wakazi wa jiji la Nairobi watakuwa wenyeji wa mkutano wa mwisho wa BBI ambao utaandaliwa katika uwanja wa Uhuru Park mwisho wa mwezi huu.