Uhuru hatafika Nakuru kwa mkutano wa BBI
K’ONYANGO na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta hatahudhuria mkutano wa mpango wa maridhiano (BBI) mjini Nakuru mnamo Machi 21 na mgeni wa heshima atakuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Hii ni kinyume na shinikizo za wandani wa Naibu Rais William Ruto waliomtaka Rais Kenyatta kuhudhuria mkutano huo, wakidai hawamtambui Bw Odinga.
Gavana wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos, ambaye ni mmoja wa walioteuliwa na Rais kuongoza mchakato huo katika eneo la Rift Valley, Jumatano aliambia Taifa Leo kwamba kwa kuwa BBI ni zao la muafaka kati ya Rais na Bw Odinga na “hivyo ikiwa mmoja hatakuwepo mwenzake atakuwepo.”
“Tunawajua wakuu wa handisheki na BBI. Kwa hivyo, Rais alituambia kwamba hatahudhuria mkutano wetu. Kwa hivyo, Raila ndiye atakuwa mgeni wetu wa heshima,” akasema kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo.
Bw Tolgos aliongeza kuwa Rais Kenyatta aliwahimiza kuhakikisha kuwa kila kiongozi anapewa nafasi ya kutoa maoni na mapendekezo yake katika mkutano huo ambao utakaofanyika katika uwanja wa michezo wa Afraha.
“Rais alisisitiza kuwa tuwashirikishe viongozi wote katika mkutano ambapo kila kiongozi ataruhusiwa kuzungumza bila kudhibitiwa tofauti na hali ilivyokuwa katika mikutano ya awali ambapo baadhi ya wanasiasa wenye maoni pinzani walidai kutengwa,” akaeleza.
Mnamo Jumanne Rais Kenyatta alikutana na magavana tisa kutoka Rift Valley katika Ikulu ya Nairobi kujadili mipango kuhusu mkutano huo wa BBI. Waliafikiana kwamba Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui.
Baadhi yao walikuwa; Jackson Mandago (Uasin Gishu), Profesa John Lonyangapuo (Pokot Magharibi), Nderitu Muriithi (Laikipia) Paul Chepkwony (Kericho), Stanly Kaptis (Baringo), Josephat Nanok (Turkana), Hillary Barchok (Bomet) na Stanley Kiptis (Baringo). Wenzao Stephen Sang (Nandi), Patrick Khaemba (Trans Nzoia) na Moses Lenolkulal hawakuwepo lakini wakaomba radhi.
“Mkutano wa Ikulu uliamua kwamba mwenyekiti wetu katika maandalizi awe gavana mwenyeji Bw Kinyanjui. Hatutaki mivutano isiyo na msingi kwamba endapo Raila atahudhuria ndiye ataongoza ratiba. Raila atakuwa tu mgeni mheshimiwa sawa na ilivyokuwa katika mikutano mingine ya awali,” Bw Tolgos akasisitiza.
Duru ziliambia Taifa Leo kwamba wandani wa Dkt Ruto walitaka kupata nafasi ya kumkabili Rais Kenyatta kuhusu changamoto za uongozi ndani ya chama cha Jubilee kwa sababu amedinda kuitisha mkutano wa kundi la wabunge (PG) ili kupanga uchaguzi wa chama.
Mbunge wa Keiyo Kusini Daniel Rono na mwenzake wa Soy Caleb Kositany jana walisema waliomtaka Rais Kenyatta ahudhurie mkutano wa BBI Afraha ili wapate nafasi ya kumuuliza msimamo wake kuhusu siasa za urithi ndani ya Jubilee na kitaifa.
Wabunge hao walielezea kutofuridhishwa kwao na jinsi mikutano ya awali ya BBI imekuwa ikiendeshwa, wakidai iligeuzwa kuwa mikutano ya kuendeleza sera na maongozi ya ODM.
“Mkutano wa Afraha utakuwa muhimu kweti kama viongozi wa Rift Vallet kwa sababu tutautumia kumuuliza Rais ikiwa handisheki yake na Dkt Ruto 2012 ingalipo au la. Pia tunamtaka aeleza kuhusu jinsi mikutano ya BBI imekuwa ikiendeshwa kwa sababu wakati hu inaonekana kama majukwaa ya ODM,” akasema Bw Ruto.
Bw Kositany alisisitiza kuwa ikiwa Rais atakosa kuhudhuria mkutano wa Nakuru, Naibu Rais ndiye anapasa kupokea memoranda yao “kwa sababu hatuwezi kuwasilisha hati hiyo kwa mtu tusiyemfahamu.”