• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Huenda Kenya ikawa na Naibu Rais wa kike 2022

Huenda Kenya ikawa na Naibu Rais wa kike 2022

Na MARY WANGARI

HUENDA Kenya ikawa na naibu wa rais wa kwanza mwanamke katika Uchaguzi Mkuu 2022 ikiwa mapendekezo ya Wawakilishi Wanawake 47 yaliyowasilishwa kwa jopokazi la Mpango wa Maridhiano (BBI) yatatekelezwa.

Wakiwasilisha maoni yao Jumanne katika hoteli ya Laico Regency, Nairobi, Wawakilishi hao wa Wanawake walihoji kwamba sheria ya thuluthi mbili kuhusu uwakilishaji wa kijinsia inapaswa kutekelezwa kikamilifu katika viwango vyote vya serikali.

Viongozi hao, wakiongozwa na Mwakilishi Mwanamke katika Kaunti ya Homabay Gladys Wanga na Mwakilishi wa Kaunti ya Murang’a Sabina Chege, walihoji kwamba, sheria kuhusu uwakilishaji wa jinsia imekawia kutekelezwa kikamilifu katika nyadhifa za uongozi nchini.

“Sheria ya thuluthi mbili kuhusu uwakilishaji wa jinsia imechukua muda mrefu kutekelezwa kikamilifu. Kumekuwa na majaribio matano ya kushinikiza utekelezaji wake lakini yote yameambulia patupu. Tunataka sheria hii itekelezwe kikamilifu mara moja,”

“Tunataka hali ambapo ikiwa mgombea urais atakuwa mwanamme, mgombea mwenza wake atakuwa mwanamke, vivyo hivyo kwa waziri mkuu na naibu wake hadi kwenye viwango vya kaunti ambapo ikiwa gavana atakuwa mwanamume, naibu wake awe mwanamke na kadhalika,” alisema Bi Wanga.

Aidha, viongozi hao wanataka nyadhifa za wawakilishi wanawake kudumishwa katika kaunti zote 47 nchini pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa kiwango cha 50/50 cha usawazishaji bungeni utakaohusisha wanawake, walemavu pamoja na makundi mengine yaliyotengwa.

“Manufaa yote ya wanawake kutokana na Katiba 2010 yanapaswa kusalia yalivyo bila kupotezwa. Tunapendekeza viti vyote 47 vya Wawakilishi Wanawake vidumishwe pamoja na mfumo jumuishi Bungeni kwa kiwango cha 50/50,”

Wabunge hao pia wameitaka serikali kuwezesha kuwepo kwa raslimali za kutosha ili kufanikisha utekelezaji wa Kifungu 2B kuhusu Elimu ya Msingi ikiwemo usambazaji wa sodo kwa wanafunzi wote wa kike waliovunja ungo.

You can share this post!

Uhuru hatafika Nakuru kwa mkutano wa BBI

Nambari ya Serikali ya kuripoti coronavirus yageuka...

adminleo