Watu milioni 4 hawana chakula Kenya, utafiti wafichua
Na PETER MBURU
KILA wakati thuluthi moja ya wakazi wa Kaskazini mwa Kenya wanaathiriwa na baa la njaa kiasi cha kuhitaji misaada.
Vilevile, asilimia 29.4 ya watoto walio chini ya miaka mitano nchini wanakumbwa na utapia mlo, huku asilimia 26.2 wakikosa kukua inavyostahili kiafya, kwa kukosa lishe bora.
Hii ni kulingana na ripoti iliyotolewa na shirika la utafiti wa kilimo na njaa kimataifa, Welthungerhilfe (GHI) Alhamisi, pamoja na maelezo kutoka Wizara ya Kilimo.
Mkurugenzi wa idara ya utafiti wa kilimo katika wizara ya Kilimo, Dkt Oscar Magenya alisema, japo mwaka jana wizara hiyo ilizindua mpango wa kuboresha kilimo nchini kwa miaka kumi ijayo, muundo wa mashirika na mipangilio ya utendakazi katika sekta ya kilimo nchini vimezuia mikakati ya kuboresha kilimo, na hivyo kupunguza njaa nchini.
“Haijalishi malengo tuliyo nayo ya kuboresha kilimo yalivyo kwa kuwa muundo wa mipangilio ya utendakazi ulivyo hautasaidia,” Dkt Magenya akasema.
“Kwa sasa, kila wakati kuna watu milioni 4 wasio na chakula cha kutosha nchini na serikali inashirikiana na washikadau mbalimbali ili kuwasaidia wakulima wenye mashamba wadogo, kukuza chakula cha kutosha, mbali na kuboresha viwango kabla ya kuuza,” akasema
Ripoti ya GHI ambayo imejumuisha habari kuhusu viwango vya njaa katika mataifa 117 duniani mwaka jana iliorodhesha Kenya ya 86 kwa athari za njaa, ikitaja hali ya njaa nchini kuwa ya kutisha.
Aidha, Kenya iliorodheshwa kati ya mataifa 45 ambayo kufikia 2030 hayatakuwa yameafikia viwango vya chini vya njaa ilivyokuwa imetarajiwa, kulingana na hatua ambazo zimekosa kuchukuliwa mbeleni kukabiliana na hali hiyo.
Sababu kuu ya njaa ilibainishwa kuwa mabadiliko ya hali ya anga duniani, ambayo yamekuwa yakipunguza mazao ya mimea, pamoja na kusababisha majanga yanayoathiri uzalishaji wa vyakula, na hivyo utoshelezaji wa chakula.
“Kulikuwa na kiangazi 2017, 2018 na 2019 na katikati ya misimu ya kiangazi kukawa na mafuriko, sasa kuna uvamizi wa nzige, vyote ambavyo vinaathiri uzalishaji wa chakula. Baadhi ya jamii bado hazijarejelea hali ya kawaida kimaisha kutokana na majanga ya awali, hivyo yakisukumwa katika hali ya hatari,” akasema mkurugenzi wa shirika la Welthungerhilfe humu nchini, Kelvin Shingles.
Alisema kuwa Kaskazini mwa Kenya ndiko kumeathirika zaidi kutokana na majanga hayo, pamoja na vita vya kijamii na ukosefu wa uhusiano mwema na jamii za mataifa jirani.
“Thuluthi ya wakazi wa Kaskazini mwa Kenya wana njaa inayohitaji misaada ya vyakula na kusaidiwa katika mahitaji mengine ya kimsingi,” Bw Shimbles akasema.
Kulingana na ripoti hiyo, Jamhuri ya CAR ndiyo imeorodheshwa kuwa na viwango vya juu zaidi vya njaa duniani, hali yake ikitajwa kuwa mbaya zaidi siku sijazo.
Nchi za Madagascar, Yemen, Zambia na Chad zilifuata kwa viwango vya juu vya njaa duniani, huku Kenya na mataifa mengine 42 yakishikilia nafasi ya tatu kutoka mwisho, na ambayo hali zao bado ni za kusikitisha.