Korti yatupa kesi ya uchochezi dhidi ya Kuria

Na Richard Munguti

MAHAKAMA Alhamisi ilitupilia mbali kesi ya uchochezi dhidi ya Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

Bw Kuria aliachiliwa huru na Hakimu Mwandamizi Kennedy Cheruiyot, aliyesema sheria iliyotumika kumfungulia mashtaka mbunge huyo imeharamishwa na Mahakama Kuu.

Bw Kuria, aliyekabiliwa na shtaka la uchochezi na matamshi ya kuzua hisia za chuki, alikuwa ameomba korti imwachilie kufuatia uamuzi wa Majaji Jessie Lesiit, John Mativo na Luka Kimaru.

Majaji hao waliharamisha kifungu nambari 96 cha sheria za uchochezi kilichotumika kumshtaki Bw Kuria.

Kuachiliwa kwa Bw Kuria kumefikisha idadi ya wanasiasa walioachiliwa baada ya sheria hiyo ya uchochezi kuondolewa hadi wanne.

Wengine walioachiliwa ni Mbunge wa Makadara George Aladwa, aliyekuwa Gavana wa Machakos Johnson Muthama na mwanaharakati Japheth Muroko.

Kwingineko, afisa wa polisi alishtakiwa jana kwa mauaji ya mwendeshaji bodaboda katika hospitali ya Mama Lucy jijini Nairobi.

Wakati huo huo mlinzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi anayeshukiwa alimuua mwanafunzi, atakaa rumande ili kuwapa polisi muda wa kukamilisha uchunguzi.

Afisa huyo wa polisi, Zadock Ochuka, alikanusha shtaka la kumuua mwendeshaji bodaboda aliyekuwa amempeleka mgonjwa katika hospitali hiyo ya Mama Lucy.

Mshtakiwa aliagizwa azuiliwe katika gereza la Industrial Area hadi Septemba 22, 2020 kesi itakaposikizwa.

Katika kisa cha mauaji chuoni Nairobi, bawabu kwa jina Spencer Kipkorir Kosgey alifikishwa kortini kwa mauaji ya mwanafunzi Elisha Odeng almaarufu Ras.

Mshukiwa huyo aliagizwa azuiliwe katika kituo cha polisi kuhojiwa na hatimaye kushtakiwa kwa mauaji hayo.

Hakimu mkazi Bw David Ndungi aliombwa amzuilie mshukiwa huyo kwa muda wa siku 10 kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi dhidi ya Kosgey.

Maiti ya mwanafunuzi huyo iliokotwa katika bustani iliyoko kwenye chuo hicho.

Uchunguzi ulibainisha Ras alinyongwa baada ya kuchapwa na kifaa butu.

Mlinzi huyo alikamatwa usiku wa Machi 4, 2020 na kuzuiliwa katika kituo cha Polisi cha Central kuhojiwa.

Ripoti ya upasuaji ilibaini Ras aliuawa.

Upande wa mashtaka ulipinga mshukiwa huyo akiachiliwa ukidai atavuruga ushahidi.

Wakili Felix Kiprono Matagei alipinga ombi la kumzuilia mshukiwa huyo huku akiomba aachiliwe kwa dhamana.

Mahakama itaamua ikiwa Kosgey ataachiliwa kwa dhamana.