Habari Mseto

‘Hii ndiyo dhamira ya Waititu kuingia Kanu’

March 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

MERCY KOSKEY na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu, Bw Ferdinand Waititu Babayao sasa yuko mbioni kujinusuru kisiasa kwa kukigura chama cha Jubilee na kujiunga na Kanu.

Mnamo Alhamisi gavana huyo aliyeng’olewa mamlakani Februari alikuwa kwenye ujumbe wa wanasiasa 1,500 kutoka eneo la Mlima Kenya waliomtembelea Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi nyumbani kwake Kabarak.

“Nimerejea katika chama cha Kanu ambacho nimewahi kikuhudumia kama mwenyekiti wa tawi wakati ambapo kilikuwa kingali na nguvu. Ninaamini umaarufu huo utarejea sasa chini ya uongozi wa kuanzia sasa ambapo nimejiunga rasmi,” akasema.

Bw Waititu akaongeza: “Ninaamini tutaweka mikakati kabambe itakayotuwezesha kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.”

Viongozi hao ambao walijumuisha wabunge wa sasa na wa zamani waliapa kuunga mkono azma ya Seneta huyo wa Baringo ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Kundi hilo lilikuwa na wajumbe kutoka kaunti za Nyeri, Kiambu, Murang’a, Nyandarua, Embu, Meru, Laikipia na Tharaka Nithi.

Miongoni mwao walikuwa Seneta Ephraim Maina (Nyeri), Gathoni wa Muchomba (Mwakilishi Mwanamke wa Kiambu), aliyekuwa Mbunge wa Laikipia Kaskazini Mathew Lempurkel, mwanasiasa wa Laikipia Maina Njenga, miongoni mwa wengine.

Alichukua fursa hiyo kumwalika Bw Gideon alizuru eneo la Mlima Kenya huku akiahidi kumtembeza katika kila eneobunge.

“Tembelea eneo la Mlima Kenya na Nairobi utafute kura. Niko tayari kukutembeza katika kila eneo bunge na wadi kwa sababu, inavyojua mimi ni mwanasia mwenye ushawishi mkubwa zaidi katika maeneo hayo,” Bw Waititu akaeleza.

Wadadisi wanasema mwanasiasa huyo ambaye anakabiliwa na kesi ya ufisadi mahakamani, amejiunga na Kanu ili ajinuru kisiasa baada ya kupokonywa wadhifa wake wa ugavana.

“Ninadhani kile ambacho Bw Waititu anafanya ni kujifufua upya kisiasa wakati huu ambapo nyota yake inaendelea kudidimia baada ya kuondolewa mamlakani kama gavana wa Kiambu. Anataka kutumia Kanu na jina la Gideon kujitakasa,” mchanganuzi wa siasa Reuben Nasibo.

“Na hii ndiyo maana Bw Waititu alimminia sifa Seneta Moi akimtaja kama kiongozi ‘safi’ asiye na doa lolote la ufisadi,” anaongeza.

Aidha, Bw Nasibo anafasiri hatua ya Bw Waititu kutangaza kuunga mkono mpango wa maridhiano (BBI) na kumsifia Rais Uhuru Kenyatta, kama sehemu ya mkakati wake wa kujiondoa katika kivuli cha Naibu Rais William Ruto.

Bw Waititu amekuwa mwandani wa karibu wa Dkt Ruto hadi alipoondolewa mamlakani baada ya maseneta kuidhinisha hoja iliyopitishwa katika bunge la Kiambu Desemba 19, 2019.