• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
BBI inawagawanya Wakenya, Kamishna wa NCIC sasa atahadharisha

BBI inawagawanya Wakenya, Kamishna wa NCIC sasa atahadharisha

Na TITUS OMINDE

KAMISHNA wa Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) Dkt Joseph Nasongo Wamocha ametahadharisha wanasiasa dhidi ya kutumia BBI kugawanya Wakenya.

Dkt Wamocha alisema tabia hiyo ina uwezo wa kuchochea uhasama wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi wa 2022.

Dkt Wamocha aliwataka viongozi kutoka pande zote mbili kuhubiri injili ya uvumilivu na msamaha kupitia kwa BBI.

Alisema kuwa maoni ya Wakenya wote kwa BBI ni muhimu bila kujali pande zao za kisiasa na kabila.

“Mtazamo wangu ni kwamba nchi ya Kenya inaelekea katika njia ya kisiasa telezi. Ni muhimu kutambua kuwa siasa za Kenya zinaegemea katika pande za kikabila. Kwa hivyo, viongozi wakuu wanapozozana jamii zao huchukulia kana kwamba ni kabila lao linaloandamwa, ” alionya Dkt Wamocha.

Kamishna Wamocha aliwasihi wanasiasa wasigawanye Wakenya kutokana na tamaa zao za ubinafsi.

Aliwasihi waachane na kiburi chao na kukumbatia roho ya asili ya BBI.

“Viongozi wanapaswa kuachana na tamaa na kiburi kwa kujitakia makuu ili kuepusha migogoro na vurugu ambayo inaweza kusababisha uhasama miongoni mwa Wakenya,” alisema Dkt Wamocha

Msimamo wake uliungwa mkono na chama cha wanasheria LSK tawi la North Rift.

Wajumbe wa LSK ambao walizungumza mjini Eldoret wanataka wanasiasa waache kutamka maneno ya uchochezi badala yake watoe nafasi kwa wahasisi wa BBI kumaliza kazi yao na kuwapa wakenya ripoti ya mwisho.

“Nchi yetu inakaribia uchaguzi wa 2022 na ni hatari kwa amani na utulivu wa nchi hii iwapo joto la kisiasa ambalo tunashuhudia litaendelea. Hatutaki taswira ya kile kilichotokea mnamo 2007, “alisema Dennis Magare ambaye ni mwanachama wa LSK kutoka North Rift.

Bw Magare ambaye ni mtaalamu wa maswala ya upatanishi alimtaka Rais Uhuru Kenyatta na naibu Dkt William Ruto kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri amani na uvumilivu miongoni mwa wafuasi wao.

“Rais wetu na naibu wake walipewa maamlaka na Wakenya na ni lazima watumie nafasi yao kumaliza joto la kisiasa nchini ,” akasema Bw Magare

Matamshi hayo yanajiri ambapo maandamano ya kutetea naibu rais yanazidi kushuhudiwa eneo la North Rift katika miji ya Kabarnet na Eldoret

You can share this post!

Ishara Naibu Rais anakwepa vikao vya Rais

Kivumbi cha kumrithi Joho chatifuka, Mboko yumo pia

adminleo