• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
CORONA: Hakuna masomo shuleni na vyuoni

CORONA: Hakuna masomo shuleni na vyuoni

Na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta ametoa maagizo makali kwa lengo la kulinda Kenya dhidi ya ueneaji wa virusi vya corona, baada ya idadi ya walioambukizwa nchini kufika watu watatu.

Rais alitangaza shule zote kufungwa vikiwemo vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.

Watoto wanaosoma katika shule za kutwa watahitajika kubakia nyumbani kuanzia Jumatatu, kwa amri ya serikali.

Shule zote za bweni zitahitajika kufungwa ifikapo Jumatano, huku vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zikipewa muda hadi Ijumaa kufungwa.

“Nawasihi tuwe watulivu na tuepuke kueneza habari zinazoshtua,” akasema Rais, kwenye kikao cha wanahabari nje ya afisi zake zilizo Jumba la Harambee, Nairobi.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alisema wizara hiyo itatoa mwongozo leo kuhusu jinsi shule za bweni na taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu, zitakavyotekeleza agizo hilo kikamilifu.

Alisema agizo hilo litadumu kwa muda usiojulikana.

Mgonjwa wa kwanza aliripotiwa nchini Ijumaa iliyopita, na wawili wengine waliotangazwa jana walisemekana kuwa walitangamana naye. Wametengwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).

Kuna watu wasiopungua 22 wanaoaminika walitangamana na mgonjwa huyo wa kike mwenye umri wa miaka 27 ambao bado wametengwa katika Hospitali ya Mbagathi wakisubiri matokeo ya maabara kuthibitisha kama waliambukizwa.

Wakati huo huo, Rais aliagiza wageni wanaotoka katika mataifa ambako kuna maambukizi ya corona wasiruhusiwe kuingia nchini kuanzia Jumanne jioni. Agizo hilo litadumu kwa siku 30.

Raia wa Kenya ambao wako katika nchi zilizoathirika, wataruhusiwa kuingia nchini kwa sharti kwamba watajitenga kutoka kwa watu wengine kwa siku zisizopungua 14, au wajisalimishe katika vituo vya afya ili wapewe sehemu za kujitenga hadi ithibitishwe kwamba hawaugui ugonjwa huo.

Kufikia jana, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilikuwa limeorodhesha mataifa 141 ikiwemo Kenya kuwa na watu walioambukizwa.

Shirika hilo lilisema watu 152,428 walikuwa wameambukizwa kimataifa, huku kukiwa na vifo 5,720.

Maelfu ya wengine walioambukizwa wamepona tangu ugonjwa huo ulipolipuka jijini Wuhan, China mwishoni mwa mwaka uliopita.

Rais alitaka pia wale wote walioingia humu nchini katika siku 14 zilizopita wajitenge hadi wawe na uhakika kwamba hawana virusi vya corona.

Hii ni kutokana na kuwa, imebainika ugonjwa huo unaweza kuchukua muda kabla dalili zake zianze kuonekana.

Kando na hayo, Rais Kenyatta alipendekeza kuwa kampuni ziruhusu wafanyakazi kutoa huduma wakiwa nyumbani kama inawezekana.

Hii imenuiwa kupunguza idadi ya watu wanaokaa afisini kwani njia moja ya kuzuia ueneaji wa virusi vya corona ni kwa kuepuka makongamano ya watu katika sehemu moja.

Alipendekezea umma kukoma kutumia sarafu na badala yake watumie kadi za benki au huduma za pesa kwa njia ya simu.

Katika mataifa yaliyoathirika zaidi, watafiti walibainisha mojawapo ya mbinu ambazo virusi hivyo vilienea kwa kasi ni kupitia kwa sarafu za pesa zinazopitishwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.

Rais alitaka umma kuepuka maeneo yaliyo na watu wengi ikiwemo sehemu za ibada, harusi, mazishi, maduka makuu, maeneo ya burudani na vyombo vya uchukuzi wa umma ambavyo hujaa kupindukia.

Alitoa wito kwa wahudumu wa sehemu zinazotumiwa na watu wengi kutoa dawa za kuua viini mkononi ili kulinda wateja wao dhidi ya maambukizi.

Kufikia jana, watoaji wengi wa huduma za uchukuzi wa umma hawakuwa wameanza kutoa dawa hizo kwa wasafiri jijini Nairobi licha ya kushauriwa kufanya hivyo wiki iliyopita.

You can share this post!

CORONA: Waumini wagomea ibada

CORONA: Pigo kwa wafungwa kesi zikisitishwa

adminleo