• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Gavana adai Rais hapendezwi jinsi vikao vya BBI huendeshwa

Gavana adai Rais hapendezwi jinsi vikao vya BBI huendeshwa

Na OSCAR KAKAI

GAVANA wa Kaunti ya Pokot Magharibi, Prof John Lonyangapuo amedai kwamba Rais hapendezwi na jinsi mikutano ya kuhamasisha Mpango wa Maridhiano (BBI) ilivyokuwa ikiendeshwa nchini.

Prof Lonyangapuo alisema magavana wa Rift Valley walipokutana na Rais katika Ikulu wiki iliyopita, aliwafahamisha kwamba ana malengo mazuri wala si siasa zinazozingira mikutano hiyo ambayo huongozwa na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Gavana huyo alimtetea Rais kuhusu mchakato huo akisema kuwa vile Rais anachukulia na kuelewa mchakato huo ni kinyume na vile mikutano ya BBI inafanywa.

Alipuuzilia mbali ripoti za baadhi ya vyombo vya habari kuwa magavana wa eneo la Kaskazini mwa Rift Valley waliitwa ili wapatane kupanga mkutano wa BBI uliotarajiwa kufanywa mnamo tarehe 21 katika kaunti ya Nakuru.

“Sisi wenyewe tulijipeleka kwenye ikulu. Hatukualikwa. Tulijikusanya kama magavana na tukaamua kuenda kumuona Rais,” alisema.

Akiongea na wanahabari mjini Kapenguria, alisema kuwa viongozi wa Bonde la ufa watakutana tena kabla ya Machi 21 kupanga mikakati.

“Tulikuwa tukutane tarehe 19 tuangalie mapendekezo ambayo tutawasilisha kwa jopo la maridhiano. Tunataka kuhakikisha kuwa kuna usalama mapendekezo kwenye ripoti hiyo yetu yatachukuliwa kwa uzito,” alisema .

Prof Lonyangapuo alisema kuwa wakazi wa eneo la Rift Valley wanafaa kupewa nafasi ya kuwasilisha mapendekezo yao bila kutatizwa na maazimio ya kibinafsi ya wanasiasa.

“Wale ambao wanatoka maeneo ya nje wanafaa kuketi na kusikiza. Tunaishi kwa amani na jamii zote za Bonde la Ufa,” alisema.

Mkutano wa Nakuru uliahirishwa baada ya Wizara ya Afya kutangaza kuna mgonjwa wa virusi vya corona nchini mnamo Ijumaa.

You can share this post!

CORONA: Mvutano ufuoni polisi wakikataza wakazi kuogelea

CORONA: Hakuna Pasaka kanisani, misa zote zitapeperushwa...

adminleo