• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
CORONA: Tanzania, Somalia zaripoti visa vya kwanza

CORONA: Tanzania, Somalia zaripoti visa vya kwanza

NA MASHIRIKA

Tanzania na Somalia ni mataifa ya hivi punde kuripoti visa vya virusi vya corona katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Wizara ya Afya ya Tanzania ilitangaza kwamba abiria mwanamke mwenye umri wa miaka 46 aliyepatikana na virusi hivyo, alisafiri kutoka Ubelgiji kupitia ndege ya Rwanda iliyotua katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) Jumapili.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema mwanamke huyo aliondoka Tanzania Machi 3 na kutembelea Uswidi na Ujerumani kabla ya kuelekea Ubelgiji kisha kurejea nyumbani wikendi.

“Baada ya kuwasili KIA, kiwango cha joto mwilini mwake kilikuwa kawaida. Hata hivyo, hakuna dalili zozote zilizoonekana na ikabainika alihitaji vipimo zaidi,” akasema Mwalimu.

Mwanamke huyo kwa sasa anaendelea kutengwa katika hospitali ya Mount Meru.

“Alinieleza kupitia mazungumzo ya simu kwamba alikuwa akiishi kwenye nyumba ambayo mmiliki wake alikuwa na virusi vya corona alipokuwa Ubelgiji. Alifanyiwa vipimo katika maabara ya kitaifa iliyothibitisha kwamba ana virusi,” akasema.

Mwalimu, hata hivyo, aliwataka raia wa Tanzania kuwa watulivu huku serikali ikiendelea kuweka mikakati ya kuzuia ueneaji wa virusi vya corona.

“Chanzo cha kisa hiki ni nje ya nchi ila serikali imeweka mikakati maridhawa ya kudhibiti hali,” akasema.

Wizara ya Afya ya Somalia nayo ilisema raia wake aliyekuwa na virusi hivyo alikuwa amesafiri kutoka China.

“Serikali imethibitisha kisa cha kwanza cha corona nchini. Mwaathiriwa aliingia nchini kutoka China jana,” ikasema taarifa ya wizara hiyo.

Waziri wa Usafiri wa Angani, Abdullahi Salad Omaar alithibitisha kisa hicho na kutangaza kuwa Somalia imefutilia mbali safari za kimataifa za ndege kwa muda wa siku 15 kuanzia leo.

Kufikia jana watu 6,685 walikuwa wameaga dunia kutokana na virusi hivyo. Wengine 174,561 walikuwa wameambukizwa huku watu 77, 866 wakitibiwa na kupona virusi hivyo vilivyoripotiwa mara ya kwanza jijini Wuhan, China, Desemba mwaka jana.

Kwingineko, huku virusi vya corona vikiendelea kuathiri mataifa mengine duniani, Israel bado inaendelea kukabiliwa na utata wa kisiasa unaohusisha Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na mpinzani wake Benny Gantz.

Virusi vya corona vimeambukiza raia 250 wa Israel japo hakuna mauti yoyote yaliyoripotiwa huku raia wengine wakichukua tahadhari na kujitenga ili kuzuia maambukizi zaidi. Nchi hiyo pia imepiga marufuku mikutano inayozidi watu 10 na kuagiza shule, vyuo vikuu na mikahawa ifungwe kutokana na virusi hivyo.

Rais Reuven Rivlin ametoa wito kwa Netanyahu na Gantz waunde serikali haraka ili kusaidia katika uimarishaji wa juhudi za kupigana na kuenea kwa virusi vya corona nchini humo. Kumekuwa na mazungumzo ili wawili hao waunde serikali ya pamoja lakini misimamo yao mikali imezuia hilo kuafikiwa.

Hapo jana, Gantz ambaye anaongoza chama cha Blue and White alipewa siku 42 kuunda serikali na Rais Rivlin lakini wadadisi wa kisiasa wametabiri kwamba hatafanikiwa kutokana na mgawanyiko ndani ya vyama vya Kiarabu vinavyomuunga mkono.

Netanyahu ambaye ni Waziri Mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi Israel jana alisema kwamba wapigakura walimpa nafasi ya kuendelea kushikilia wadhifa huo kwenye uchaguzi wa Machi 2. Hata hivyo, utawala wake umezingirwa na ufisadi na kuzua malalamishi kati ya wapinzani wake kwamba anafaa kujiuzulu.

Uchaguzi wa Machi 3 ulikuwa wa tatu kuandaliwa nchini humo ndani ya mwaka moja. Chama cha Likud ambacho kinaongozwa na Netanyahu kilishinda viti 58 huku kile cha Blue and White chake Gantz kikishinda viti 36. Hata hivyo, Gantz atakuwa na uwezo wa kuunda serikali iwapo atapigiwa kura na vyama vya Kahol Lavan na Joint List vyenye wabunge 33 na 15 mtawalia.

Netanyahu, 70 mnamo Jumapili alipendekeza kubuniwa kwa serikali ya muungano kwa muda wa miezi sita ili kusaidia katika kupambana na virusi vya corona. Pia alipendekeza serikali ya muungano kwa muda wa miaka minne ambapo watagawanya majukumu yanayotekelezwa na Waziri Mkuu.

Hata hivyo, Gantz alikataa pendekezo hilo, akisema hawezi kuhudumu kwenye serikali pamoja na Netanyahu ambaye anakabiliwa na kesi ya kufuja mali ya umma.

You can share this post!

CORONA: Tahadhari kwa abiria

Corona yaua kocha

adminleo