Habari Mseto

Ombi lingine tatanishi kuhusu urais latua bungeni

April 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

OMBI tata la kuongeza muhula wa wabunge hadi miaka sita na kupunguza muhula wa rais hadi miaka minne liliwasilishwa bungeni Alhamisi.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi aliaamuru Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) kushughulikia mapendekezo, mengine ya kiajabu, kwenye ombi ambalo limewasilishwa na raia wa kawaida.

Aidha, katika ombi hilo, Ezekiel Njeru kutoka kaunti ya Embu anataka katiba ifanyiwe mabadiliko ili kuongeza maeneo bunge kutoka 290 hadi 300, kuondoa nyadhifa za maseneta na madiwani maalum wa kike huku akipendekeza kuwa lugha za kiasili zitumike katika mijadala bungeni.

“Ombi hili la mkazi wa Embu, Bw Ezekiel Njeru ni lenye uzito mkubwa kwani mapendekezo yake yatahitaji mabadiliko makubwa katika katiba ya sasa, hatua ambayo itahitaji kuandaliwa kura ya maamuzi,” akasema Bw Muturi kabla ya kuanza kusoma mapendekezo hayo.

“Mkenya huyo anataka kipengee cha 89 cha katiba kuhusu mipaka kifanyiwe mabadiliko ili kuongeza idadi ya maeneo bunge kutoka 290 hadi 300 na hitaji la uhitimu wa masomo liondolewe; kipengee cha 136 kuhusu uchaguzi wa rais ili muhula wake wa kuhudumu upunguzwe kutoka miaka mitano hadi minne huku ule wa wabunge uongezwe kutoka miaka mitano hadi sita.

“Vile vile, anataka maseneta wahudumu kwa muhula mmoja wa miaka saba pekee na nafasi 20 za maseneta maalum wa kike pamoja na madiwani 774 maalum wa kike ziondolewe. Bw Njeru pia anataka kipengee cha 120 (1) kuhusu lugha rasmi bunge kifanyiwe mabadiliko ili lugha za kiasili zitumike bungeni,” akasema Bw Muturi.

Spika Muturi aliipa JLAC inayoongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini William Cheptumo kulichanganua ombi hilo kwa siku 60 kisha kuwasilisha ripoti bungeni.

“Ombi hili sasa litashughulikiwa na JLAC itakayohitaji kumwalika Bw Njeru kufika mbele yake ili atetee mapendekezo yake,” akasema.

Baadhi ya wabunge walisikika wakichangamkia baadhi ya mapendekeo hasa yale ya kuongeza muhula wao na hitaji la masomo huku wengine wakinung’unikia wazo kwamba lugha za kienyeji zitumike katika mijadala bungeni.

Pendekezo la kuongezwa kwa idadi ya maeneo bunge linajiri wiki moja baada ya Kiongozi wa chama cha ThirdWay Ekuru Aukot kuzindua kampeni ya kushinikiza mabadiliko ya katiba kupunguza idadi ya wabunge na maseneta waliochaguliwa kutoka 338 hadi 194.

Aidha, anapendekeza kufutiliwa mbali kwa nyadhifa 47 za Wabunge Wawakilishi wa Kaunti, kama sehemu ya kupunguza gharama ya mishahara ya maafisa wa umma.

Akizindua kampeni ya ukusanyaji wa sahihi kufanikisha kuandaliwa kwa kura ya maamuzi kufanikisha lengo hilo, Bw Aukot alisema idadi ya sasa ya wabunge ni juu zaidi.

“Bunge letu lina wabunge wengi kupita kiasi kwamba baadhi yao huwa hawaachangii mijadala bungeni. Huu ni mzigo kwa mlipa ushuru kwa sababu mishahara wanayolipwa haileti faida yoyote kwa Wakenya,” akasema huku akiongeza kuwa baadhi ya wabunge wanaunga mkono pendekezo.