• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Ofisi kadhaa za serikali zafungwa mjini Thika

Ofisi kadhaa za serikali zafungwa mjini Thika

Na LAWRENCE ONGARO

MJI wa Thika umegeuka kuwa kama mahame baada ya kushuhudia idadi ya watu wachache wakiendesha shughuli zao.

Baadhi ya ofisi za serikali tayari zimefungwa huku kwenye malango kukiwa tu na mabawabu na ilani za kuonyesha maelezo ya kusitishwa kwa muda baadhi ya shughuli.

Magari ya uchukuzi hasa matatu pia ni machache ikilinganishwa na wingi wa wanafunzi wanaorudi nyumbani baada ya serikali kuamrisha warejee kwao kama njia mojawapo ya kukabili maambukizi ya COVID-19.

Wanafunzi wengi wameonekana njiani na barabarani wakirudi nyumbani huku wakitafuta njia ya usafiri.

Wengi wamekusanyika katika vituo vya matatu.

Wanafunzi hao wameonyesha nyuso za furaha kurejea nyumbani huku wakisukumana kuingia kwenye matatu.

Baadhi ya ofisi zilizofungwa kwa muda ni Mahakama Kuu ya Thika ambayo imetoa ilani ikisema ya kwamba watafunga kwa wiki mbili.

Kuna pia ofisi ya ardhi, ofisi ya mamlaka ya usalama barabarani (NTSA), ofisi ya elimu ya DEO, na ile ya idara ya watoto.

Katika ofisi ya Naibu Kamishna kuna maafisa wachache tu ambao bado wanaendelea kuhudumia wananchi.

Watu wengi wamekosa kupata huduma muhimu katika ofisi kadhaa za serikali hasa waliokuwa hawana ufahamu kuwa ilani ilitolewa kusitisha shughuli kadhaa kwa muda.

Biashara nyingi pia zinahofia kufunga hivi karibuni wakihofia kukosa wateja huku COVID-19 ikizidi kuleta hofu ulimwenguni kote.

“Mambo yakiendelea hivyo pengine tutalazimika kufunga biashara zetu hasa sisi tunaoendesha hoteli. Tumeanza kuona ya kwamba wateja wanapungua kila siku,” amesema Henry Kimani ambaye anaendesha biashara ya hoteli mjini Thika.

Wafanyakazi wengine wanahofia pengine kibarua chao kinaweza kukatika kufuatia janga hilo la COVID-19.

“Tunaendelea kuomba Mungu janga hili liishe ili tuendelee na shughuli zetu za kawaida. Sisi tunaofanya kazi katika viwanda na sehemu zingine tungetaka kusitokee uamuzi wa kufuta watu kazi,” amesema Francis Kimani, ambaye ni mfanyakazi katika kiwanda kimoja mjini Thika.

Kuna watu wanaotegemea kazi za vibarua ambao wanasema hawawezi kuvumilia kuketi nyumbani hata siku moja kwa sababu wamezoea kufanya kazi ya kulipwa kila siku.

You can share this post!

Kenya sasa ina visa 4 vya Covid-19

Thiwasco yashirikiana na kaunti kuweka vituo vya usafi Thika

adminleo