MAKALA MAALUM: Mama wa Taifa waliojaliwa kuliko wengine duniani
Na FAUSTINE NGILA
MNAMO Aprili 17, 2018, Bi Barbara Pierce Bush, mkewe mmoja wa waliokuwa marais wa Amerika na mama ya rais mwingine, aliyetambulika kwa kupigania elimu kwa wote alifariki dunia nyumbani kwake jijini Houston, akiwa na umri wa miaka 92.
Wakati wa kifo chake, mumewe ambaye ni rais wa zamani wa taifa hilo, George H W Bush, aliyekuwa pembezoni mwa kitanda cha hospitali alikolazwa, alimshika mkono kwa siku nzima kulingana na taarifa iliyotolewa na familia hiyo iliyosema Bw Bush ‘alivunjika moyo.’
Mwanawe Barbara Bush, George W Bush alisema, “Kwetu sisi alikuwa muhimu sana. Mama alitulea vizuri na kutuchekesha hadi kifo chake. Mimi ni mwanamume mwenye bahati sana kuwa mwanawe Mama wa Taifa wa zamani, Barbara Bush. Familia yetu itamkosa sana, na tunawashukuru kwa maombi yenu.”
Tofauti na mama wengi wa taifa duniani, Bi Barbara Bush alibahatika kuwa mume wa rais na pia kumzaa rais.
Mumewe, George H W Bush alikuwa rais wa Amerika kati ya mwaka 1989 hadi 1993 huku mwanawe George W Bush akiongoza taifa hilo kati ya 2001 na 2009.
Lakini si mwanamke huyu pekee aliye na bahati hii ya kipekee duniani. Hapa barani Afrika kuna wanawake wengine pia walioolewa na marais na wanao kuchaguliwa rais. Taifa Leo inaangazia mataifa hayo ambako bado wanawake hao wako hai.
- Mama Ngina Kenyatta – Kenya
Mamaye Rais wa sasa wa Jamhuri ya Kenya, Bw Uhuru Kenyatta, Mama Ngina Kenyatta, alikuwa mkewe rais mwazilishi wa nchii hii, Mzee Jomo Kenyatta.
Mzee Kenyatta alitawala kuanzia mwaka 1964 hadi kifo chake mwaka 1978. Miaka 35 baadaye, mwanao wawili hao waliyemzaa 1961, Uhuru Kenyatta, alishinda uchaguzi wa urais na kuingia Ikulu hapo 2013. Rais Kenyatta alishinda tena katika Uchaguzi Mkuu wa 2017 na ataongoza hadi 2022, kipindi chake kitakapotamatika.
- Sifa Mahanya – Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
Wakati mama wa taifa wa zamani wa taifa hili, Sifa Mahanya aliolewa na mwanamapinduzi machachari Laurent-Desire Kabila, hakutarajia kamwe kuwa mumewe angekuwa rais kwa wakati mmoja (1997) na mwanawe kuchukua hatamu za uongozi wa taifa hilo lililoko katikati ya Afrika.
Laurent Kabila aliuawa na mlinzi wake Rashidi Muzele alasiri ya Januari 16, 2001 ambaye pia aliuawa kwa kupigwa risasi wakati akijaribu kuhepa makazi ya rais huyo ya Palais de Marbe.
Mwili wake Kabila ulisafirishwa hospitalini nchini Zimbabwe huku serikali ikidai bado alikuwa hai. Hatimaye ilisema alifariki kutokana na majeraha na mwili wake kurejeshwa nchini DRC wiki moja baadaye.
Baada ya siku nane, mwanawe Laurent Kabila na Sifa Mahanya, Joseph Kabila alikabidhiwa mamlaka ya urais. Ameongoza taifa hilo tangu Januari 2001 hadi sasa.
- Mama Fatma Karume – Zanzibar
Raia wa Uganda John Okello aliongoza mapinduzi ya kipekee yaliyotia kikomo utawala wa waarabu kisiwani Zanzibar, na kumualika mwanasiasa wa kisiwa hicho aliyetambulika zaidi, Abeid Amani Karume kuwa rais mwaka 1964.
Rais Karume alikuwa ashamuoa Bi Fatma Karume na pamoja wakajaliwa watoto wawili wa kiume – Ali Karume na Amani Abeid Karume.
Ingawa rais huyo mwanzilishi aliuawa kwa kupigwa risasi na majambazi wanne wakati akicheza bao katika makao makuu ya chama cha Afro Shiranzi, Zanzibar Aprili ya mwaka 1972, miaka 28 baadaye mwanawe alichaguliwa kuwa rais.
Amani Abeid Karume aliongoza nchi hiyo kutoka Novemba 2000 hadi 2010 mwezi sawa.
- Patience Dabany – Gabon
Rais wa zamani wa Gabon, El Hadj Omar Bongo Ondimba, anatambulika zaidi hapa barani Afrika kama rais aliyekwamilia mamlaka ya urais kwa muda mrefu zaidi, miaka 42.
Katika kipindi hicho alioa wake watatu – Edith Lucie Bongo (1990–2009), Patience Dabany (1959–1986), Louise Mouyabi Moukala (1955–1959), lakini ni Patience Dabany aliyebahatika zaidi kwa kuwa licha ya kutengana na mumewe 1986, mwanawe, Ali Bongo Ondimba ndiye rais wa sasa wa Gabon baada ya kuingia Ikulu hapo 2009.
Mumewe Dabany aliongoza taifa hilo kutoka 1967 hadi 2009 alipofariki.
- Sena Sabine Mensah – Togo
Aliyekuwa rais wa Togo, Gnassingbé Eyadéma alifaulu katika mapinduzi mawili ya kijeshi – Januari 1963 na Januari 1967 na hatimaye kuwa rais Aprili mwaka huo.
Mkewe rais huyo, Sena Sabine Mensah alikuwa Mama wa Taifa kwa miaka 38 hadi kifo cha mumewe hapo Februari 2005 kilichotokana na mshtuko wa moyo jijini Tunis, Tunisia.
Lakini familia hiyo iliendelea kuongoza taifa hilo kwani mwanawe Sena na Gnassingbe, Faure Essozimna Eyadéma aliridhi urais kutoka kwa babake pindi tu baada ye kifo chake 2005. Ametawala hadi sasa.
- Lalla Latifa – Morocco
Mfalme Hassan II aliongoza taifa la Morocco kuanzia 1961 hadi kifo chake 1999. Katika kipindi hicho, alikuwa na wake wawili – Lalla Fatima na Lalla Latifa.
Mnamo Agosti 1964, mfalme huyo na mke wake wa pili, Lalla Latifa, walijaliwa mtoto wa kiume ambaye alichukua hatamu za uongozi wa taifa hilo baada ya kifo cha baba yake mnamo 1999. Amekuwa kiongozi wa nchi hiyo ya uarabuni hadi sasa.
- Ruth Williams Khama – Botswana
Ingawa ashafariki (2002), Mama wa Taifa wa zamani wa Botswana, mzaliwa wa Uingereza Bi Ruth Williams Khama alifurahia fursa ya kuwa muhibu wa rais ambaye pamoja walizaa rais.
Mumewe mama huyo, Seretse Maphiri Khama aliongoza serikali ya Botswana kutoka 1966 hadi 1980. Imeichukua familia hiyo miaka 28 kurudi uongozini kupitia kwa mwanawe Ian Khama aliyetawala nchi hiyo kutoka 2008 hadi mwaka huu.
Katika uchanganuzi, mama wawili wa taifa ambao wanao hatimaye walitwaa mamlaka ya urais walikuwa wameolewa kama wake wa pili – Gabon na Morocco.
Pia imezichukua familia mbili miaka 28 kurejea madarakani ya urais – Zanzibar na Botswana. Wanao marais wa zamani wa nchi nne – DRC, Gabon, Togo na Morocco waliridhi urais kutoka kwa baba moja kwa moja.