Habari Mseto

CORONA: Polisi watimua waumini wakaidi makanisani

March 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

POLISI mjini Mombasa Jumapili walilazimika kutimua waumini waliokaidi ushauri wa Serikali Kuu na kuendelea na ibada makanisani.

Katika kanisa la Jesus Celebration Center (JCC) eneo la Buxton, waumini waliokuwa wamejitayarisha kuhudhuria misa ya pili walilazimika kurudi nyumbani, polisi walipoweka ulinzi mkali katika lango la kanisa hilo, huku wakiwazuia waumini kuingia ndani.

Tawi la kanisa la JCC lililoko Bamburi pia lilikuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, ambao baadaye walitimua waumini waliotaka kuhudhuria misa ya pili.

Kamanda wa Polisi Kisauni, Bw Julius Kiragu, alisema kanisa hilo lilienda kinyume na agizo la serikali.

Katika kanisa la Zion Fire Ministries Changamwe, polisi walilazimika kuwatimua waumini walipokataa kutii agizo la kufunga kanisa baada ya misa ya kwanza.

“Tuliwapa wakati wa kumaliza misa ya kwanza na kuwaeleza waende nyumbani. Lakini waliamua kuendelea na misa ya pili. Ndio maana tukawatimua,” alisema kamanda wa polisi Changamwe, Bw Issa Mohammed.

Hata hivyo, polisi wanasema hakuna muumini yeyote aliyejeruhiwa katika shughuli hiyo.

Kasisi wa Kanisa la Kisima cha Neema, Mshomoroni Mary Kagendo, aliiomba serikali ikubali maombi katika makanisa kuendelea.

“Ni muhimu kwa kutatua janga ambalo linashuhudiwa nchini,” akasema.

Katika eneo la Shika Adabu, Likoni, Chifu Athuman Mwakashi aliongoza manaibu wake kuzuia ibada zilizokuwa zikiendelea, huku baadhi ya waumini wakidai walikuwa wakitekeleza matakwa waliyoagizwa na serikali kama njia za kuzuia maambukizi.

Katika kanisa la Life Way Pentecoastal Church, Ujumaa, machifu hao walikuwa na wakati mgumu wa kujaribu kuwahamasisha waumini haja ya kufanyia ibada zao nyumbani jinsi ilivyoagiza serikali.

Naibu Kamishna wa Likoni, Bw Francis Kazungu aliwataka wakazi wa eneo hilo wazingatie maagizo ya serikali, ili kuzuia uwezekano wa maambukizi ya virusi vya corona.

Wavuvi nao waliendelea na shughuli zao maeneo tofauti ya uvuvi katika kaunti, kukiwa hakuna vifaa vya kujikinga kama sabuni na maji safi.

Katika eneo la uvuvi la Ngare, Portreitz, wengi walinawa mikono wakitumia maji ya chumvi kutoka baharini bila kutumia sabuni.

Akizungumza na Taifa Leo, mwenyekiti wa eneo la uvuvi la Ngare, Bw Abdallah Kitondo, alisema kuwa wavuvi hawawezi kubakia nyumbani.

“Hatuwezi kufanyia kazi zetu nyumbani. Tukikaa nyumbani tutakula nini? Kama serikali ingekuwa na mpango wa kutoa chakula kwetu, labda tungebakia nyumbani. Tunaamini viini havikai katika maji ya chumvi,” akasema.

Naye mwenyekiti wa eneo la uvuvi la Old Town, Bw Swaleh Mohammed, alisema kuwa wavuvi wananawa mikono kutumia maji ya bahari ambayo yana chumvi.

Alisema ni vigumu kupunguza idadi ya wavuvi katika boti za kuvulia samaki. Hata hivyo, alisema kuwa amewaagiza wavuvi wasikaribiane, wakae umbali wa mita moja.

Boti moja linaweza kubeba wavuvi watatu hadi wanane kulingana na urefu wake.

“Bado hatuna maji safi na sabuni lakini tumeomba wavuvi na wachuuzi wanaofika katika eneo hili wasikaribiane,” akasema Bw Mohammed.

Taarifa za Siago Cege, Diana Muthey na Hamisi Ngowa.